Na Gurian Adolf
Katavi
Serikali ya Mkoa wa Katavi imeonya kuwa kamwe haipo tayari kumfumbia macho mtu awaye yeyote yule atakae onyesha nia ya kuhujumu vyama vya Ushirika kwani lengo la mkoa huo ni kuendelea kusimamia ushirika imara na wenye nguvu ya kiuchumi kwa kuwahudumia wanachama wake kikamilifu.
Onyo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuga wakati akitoa hotuba yake katika uzinduzi wa jukwaa la Ushirika Mkoa wa Katavi iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Mkoa huo Kamishina wa Polisi Paulo Chagonja uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Maji mjini humo.
Alisema kuwa Serikali Mkoani Katavi itaendelea kusimamia ushirika na kamwe haitamfumbia macho mtu yeyote atakae onyesha nia ya kuhujumu vyama vya Ushirika kwa namna yoyote ile.
Lengo la Mkoa wa Katavi ni kuendelea kuwa kinara kwa kuwa na ushirika imara na wenye nguvu kiuchumi kwa kuwahudumia wanachama wake kikamilifu.
Alisema kumekuwa na malalamko kwa baadhi ya vyama vya ushirika yanayosababishwa na udhaifu katika uendeshwaji wa vyama vya ushirika na udhaifu huo umetokana na usimamizi hafifu, kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi na kukosekana kwa uwazi wa utoaji wa taarifa kwa wakati.
Chagonja alitoa rai kwa viongozi wa ushirika wa mkoa huo kufanya kazi kwa bidii,waledi uaminifu na uadilifu katika utendaji wa kazi ili mapungufu hayo yalioonekana yasitokee tena.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa kilimo cha Tumbaku kimeanza kuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupungua kwa soko au mahitaji kutoka kwa makampuni ya ununuzi na chamgamoto ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ambapo Serikali imeelekeza kuwa kila mkulima apande miti 150 katika shamba lake binafsi na kuitunza miti ya asili aina ya NIGITRI 200.
Kwaupande wake naibu mrajisi wa vyama vya ushirika Tanzania Charles Malunde alieleza kuwa vyama vya ushirika vinaweza kufa au kuporomoka kabisa endapo viongozi wanao ongoza ushirika huo watakuwa ni wabovu.
Naibu Mrajisi aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo wa jukwaa la ushirika kuwa kila mkoa unachangamoto za ushirika wapo baadhi ya watu wakiambiwa ushirika wanajua umeisha kufa na wengine wanajua kuwa Sacos sio ushirika.
Nae Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya ushirika wa Mkoa wa Katavi Luhigiza Sesemkwa alisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuingilia shughuli za vyama vya ushirika na kufanya maamuzi bila kuzingatia sheria na taratibu za ushirika.
Alisema kuwa mwamko mdogo kwa wananchi katika kujiunga na ushirika ikizingatiwa idadi ya wakazi wa Mkoa wa Katavi ni 671,194 ambapo wanachama wa ushirika ndani ya Mkoa ni 16,000 tu ambao ni sawa na asilimia 2.8 ya wananchi wote wa Mkoa wa Katavi kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
Naye Mwenyekiti wa chama cha Msingi cha Nsimbo Maganga Kasea alizilalamikia Halmashauri kwa kushindwa kutengeneza miundo mbinu ya barabara kwenye maeneo yanayozalisha Zao la tumbaku licha ya kuwa wanapata fedha nyingi zitokanazo na ushuru wa Tumbaku ambapo asilimia 5 ya thamani ya fedha za mauzo ya tumbaku huenda kwenye Halmashauri husika.
Katika uzinduzi wa jukwaa la ushirika Mkoani katavi wajumbe wa mkutano huo walifanya uchaguzi mkuu na kumchagua Moses Kabeja kuwa Mwenyekiti wa jukwaa la ushirika la mkoa wa Katavi baada ya kuwashinda wagombea watano wa nafasi hiyo na Makamu Mwenyekiti alichaguliwa Suzana Kasera aliyewashinda wagombea wanne wa nafasi hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment