Na Gurian Adolf
Sumbawanga
ALIYEWAHI kuwa mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi CCM, Sumbawanga mjini Charles Kabanga almaarufu kwa jina la Mzee Kasema amewaasa wanachama wa chama hicho kuanzia ngazi ya mkoa mpaka mashina kutowafumbia macho na kuwachagua katika nafasi mbalimbali za ndani ya chama hicho watu wote waliokisaliti chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita na kusababisha baadhi ya wanachama kukihama chama hicho.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo aliamua kutoa tahadhari kwa wanachama wenzake kutowachagua baadhi ya wanachama waliochukua fomu kwaajili ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ambao baadhi yao walisababisha chama hicho kupata upinzani mkubwa katika uchaguzi Mkuu uliopita.
Kabanga alisema kuwa wapo baadhi ya wanachama ambao walikisaliti chama hicho na hata kufikia hatua ya kukihama lakini cha kushangaza watu hao wamechukua fomu kwa nia ya kuomba nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho kitu ambacho kitakuwa ni cha ajabu kama wasaliti watapewa nafasi ndani ya chama hicho.
Alisema kuwa kutokana na utendaji kazi mzuri wa mwenyekiti wa sasa wa chama hicho taifa John Magufuli watu wengi wamevutiwa na hata kurejesha matumaini kwa chama hicho lakini tayari walionesha kuwa ni wasaliti na hawafai kupewa nafasi kwani hawaaminiki.
Kabanga ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa jumuia ya wazazi ya CCM mkoa wa Rukwa alisema kuwa mtu yeyote anaekimbia matatizo hafai katika jumuia yoyote kwani hata kama waliona kuna mapungufu katika chama hicho hawakupaswa kukimbia bali walipaswa kukabiliana na mapungufu hayo wakiwa ndani ya chama lakini kwa kitendo cha kukiambia chama hicho wanaonesha si waaminifu kwa chama hicho.
Alisema kuwa iwapo watu hao watachaguliwa huenda wakakihujumu chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao hivyo basi ni vizuri wakaogopwa kama ukoma kwani ni vigeugeu na wanaonekana huenda hata walikokimbilia wameshindwa kupata walichotarajia ndio maana wanarudi CCM.
Hata hivyo alitoa wito kwa wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi na kugombea nafasi mbalimbali kwani CCM ina wanachama wengi ambao ni wazuri na anaimani kuwa wana uwezo wa kukiongoza chama hicho bila kuwategemea hao walio onekana kuwa ni vigeu geu kutokana na kukisaliti chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mwisho
No comments:
Post a Comment