Friday, 21 July 2017

Mwalimu wa Sekondari mbaroni kwa kumpa mimba mwanafunzi wake

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MWALIMU wa shule ya Sekondari ya Miangalua wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa anatuhumiwa kumpa  ujauzito mwanafunzi wake wa kidato cha tatu na tayari anashikiliwa na jeshi  la  polisi katika kituo cha polisi cha Laela  wilayani humo.
Mwalimu huyo anayefahamika kwa jina la Florens Mbawala anatuhumiwa kumpa mwanafunzi huyo ujauzito baada ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi huyo kwa muda mrefu.
Akizungumza na gazeti hili Mkuu wa shule hiyo ya sekondari Miangalua Gishi Milundi alikiri kuwa ni kweli mwanafunzi wake ambaye anasoma kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 16 ni mjamzito na anadai kuwa amepewa ujauzito huo na mwalimu Mbawala na tayari mwalimu huyo yupo katika mikono salama ya jeshi  la polisi kwaajili ya uchunguzi.
Alisema kuwa baada ya kuhisi kuwa mwanafunzi huyo ni mjamzito alipelekwa katika zahanati ya kijiji cha Miangalua na kupimwa ndipo alipo baininika kuwa anaujauzito wa miezi mitano na yeye binafsi alikwisha muonya mwalimu huyo tabia ya kujihusisha na mapenzi na mwanafunzi huyo lakini hakusikia  mpaka alipompa ujauzito na kumsababishia kukatisha masomo kutokana na hali hiyo.
Mkuu huyo wa shule alisema kuwa yeye hana la  kufanya isipokuwa ameliachia jeshi  la  polisi ili lichukue hatua kwakua kitendo alichokifanya mwalimu huyo ni kosa kisheria na tayari amekwisha  muondoa shuleni  hapo mwanafunzi huyo kwakua Sheria haimruhusu kuendelea na masomo akiwa ni mja  mzito. 
Kwa upande wake mzazi wa mwanafunzi huyo Atanas Sokoni aliyezungumza na gazeti hili alikiri kuwa mtoto wake ni mjamzito na hivi sasa ameacha kwenda shule na kila anapoulizwa anasema kuwa ujauzito huo aliupata kutoka kwa mwalimu wake Mbawala ambaye wamekuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu.
Alisema kuwa kinacho msikitisha ni kuona kuwa mtoto wake huyo amepoteza fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari kwani serikali ilikwisha piga marufuku wanafunzi waliojifungua kurejea shuleni  ambapo alisema kua hana mpango wa kumsomesha tena kwakuwa uwezo wake ni mdogo kwani amechezea fursa ya kusoma shule za serikali itabidi akae tu nyumbani kwani hana kipato cha kumsomesha hata chuo cha ufundi yaani veta ili apate  elimu ya ufundi.
Alisema kuwa anasikitika lakini hakuna jinsi isipokuwa kulea  mjukuu kwakua tayari pia mwalimu aliyempa ujauzito anashikiliwa na polisi hivyo basi suala la  kumlea mjukuu litabaki kwake na mtoto wake ila  aliviomba vyombo vya sheria kumchukulia hatua kali mwalimu huyo ili iwe fundisho kwa walimu wengine wakware kama mwalimu Mbawala.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alisema kuwa bado mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani Mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika lakini mtuhumiwa anatuhumia kwa makosa ya kumpa mimba mwanafunzi na kumbaka kwakua mwanafunzi huyo anaumri wa chini  ya miaka 18.
Mwisho

No comments:

Post a Comment