Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAZAZI katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wameshauliwa kuwapa chakula bora watoto wao ili waweze kuondokana na tatizo la udumavu linalowakabiri watoto katika mji huo.
Akizungumza na Tabibu Dkt Godwin Kaswiza ambaye ni mganga wa kituo cha Afya cha Katandala mjini Sumbawanga alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa baadhi ya wazazi ni kutowajali watoto wao kwa kuwapa vyakula vya aina tofauti ambavyo vitawasaidia kukua vizuri na kuondokana na tatizo la udumavu linalowakabiri watoto wengi katika mji huo.
Alisema kuwa wengi wa wazazi katika mji huo wanatumia fedha zao katika mavazi, kunywa pombe na starehe nyinginezo na kusahau kabisa kuwekeza katika vyakula vya watoto wao ambao wanahitaji kukua vizuri na moja kati ya kigezo muhimu ni chakula bora.
Dkt Kaswiza alisema kuwa walau kila mzazi angejali kumpa mtoto wake hata bilauli moja ya maziwa kila siku na mayai ya kuku walau matatu kwa wiki pamoja na kumpa uji unaotengenezwa kwa unga safi wa lishe tatizo la kudumaa kwa watoto lingepungua kwa kiasi kikubwa katika mji huo.
Alisema kuwa mpaka hivi sasa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 70 ya watoto katika mkoa wa Rukwa wamedumaa lakini mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula changamoto iliyopo ni elimu ya kula kwani wazazi wamekuwa wakifikiria zaidi kuuza chakula na kupata fedha bila kufikiri kuhusu chakula cha watoto wao.
Dkt huyo alisema kuwa imefika wakati wataalamu wa lishe katika mji huo kutoa elimu ya kutosha ambapo kama jamii itapata elimu ya kutosha itasaidia pia kukabiliana na baadhi ya magonjwa yanayohitaji lishe nzuri kwani ndiyo yamekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya watoto wao ki mwili na kiakili.
Alisema kuwa wanasiasa mjini humo wanapaswa kulipa kipaumbele suala la lishe kwa wapiga kura wao kwani kama watawekeza katika lishe bora watakua na afya nzuri na wataendelea kuwapigia kura kwa muda mrefu na hata bajeti ya afya itapungua kwakua wananchi watakua na afya bora.
Naye mganga wa hospitali ya mkoa wa Rukwa Emmanuel Mtika akizungumza na gazeti la Tabibu alisema kuwa ni vizuri watu wakafundishwa namna ya kula vyakula vitakavyowapa afya nzuri kwani hivi sasa kuna tatizo la ulaji vyakula visivyofaa kwa afya hali inayochangia kuongezeka kwa magonjwa ambayo yanatokana na ulaji vyakula bila kufanya mazoezi na matokeo yake kujikuta wakipata tatizo la unene uliopitiliza.
Alisema kuwa vifo vingi hivi sasa vinatokana na magonjwa yasiyo ambukiza ambayo mengi yanatokana na utaratibu mbaya wa kula vyakula bila kufanya mazoezi na kupima afya na hii imekuwa changamoto kubwa kwani tatizo hili linazidi kukua siku hadi siku.
Mwisho
No comments:
Post a Comment