Wednesday, 26 July 2017

Mganga wa jadi auawa kwa kuchomwa mkuki na mtu anayedhaniwa kuwa ni mteja wake

Na Israel Mwaisaka
Nkasi
MGANGA wa jadi aitwaye Levocatus Kanjalanga (65) ameuawa kwa kuchomwa na mkuki mgongoni na mtu asiyefahamika ambaye anadhaniwa kuwa ni mteja wake baada ya watu ambao ni wateja wake kulalamika kwa kipindi kirefu kuwa wanatibiwa na mganga huyo ambapo anawatoza fedha nyingi na haponi maradhi yanayo wasumbua.
Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto wa mganga huyo wa jadi ambaye alikuwa anazungumza na gazeti hili alisema kuwa baba yake Kanjalanga aliuawa  Julai 25 majira ya saa 1:30 za asubuhi kwa kupigwa mkuki  mgongoni akiwa anatembea mitaani katika kitongoji cha Chawe kilichopo katika Mji wa Namanyere  wilayani humo. 
Alisema kuwa kwa muda mrefu watu ambao walikuwa wakitibiwa na mganga huyo walikuwa wakilalamika kutozwa fedha nyingi pamoja na mifugo lakini hawaponi hali iliyosababisha kuanza kumuona mganga huyo kama tapeli kutokana na kutofanikiwa matatizo yao ya kiafya,kutafuta mali pamoja na mazindiko.
Kutokana na malalamiko hayo huenda ndiyo yaliyoasababisha kuuawa kwa kuchomwa na mkuki mgongoni hadi kufariki dunia ambapo aliyefanya tukio hilo hakuweza kufahamika na anatafutwa mpaka sasa. 
Naye  Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa siku ya  Julai 23 majira ya saa 1:45 za jioni  mtembea kwa miguu , mkazi  wa Jangwani – Bomani mjini Sumbawanga aitwae Masoud Abdallah (65) aligongwa na gari na kufa papo hapo.
Alisema kuwa gari aina ya Lafecter  lenye namba za usajili T 850 DKJ likimgonga katika
eneo la Mrovarian  Center , Barabara ya Nyerere  katika Mji wa Sumbawanga.
Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe kwa upande wa dereva wa gari hilo.
 Aliongeza kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Mhasibu wa Benki ya Posta Tawi la Sumbawanga mwenye umri wa miaka(36)mkazi wa eneo la Kristu Mfalme ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi ambapo atafikishwa  mahakamni  mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Mwisho

No comments:

Post a Comment