Na Israel Mwaisaka
Nkasi
WAKAZI wa kijiji cha Mkole Kata ya Nkomolo wilayani Nkasi mkoani Rukwa wamejikuta katika taharuki baada ya Tembo wapatao 9 kuvamia kijiji chao wakitokea katika poli la hakiba la Lwafi.
Wakizungumza na rukwakwanza.blogspot.com Wananchi hao wamesema kuwa tembo hao waliingia kijijini humo jana majira ya saa 2 asubuhi ambapo wao walilazimika kujifungia ndani na watoto wao kwa kuogopa madhara endapo watakumbana na Tembo hao.
Mmoja wa Wananchi hao James Katiya alisema kuwa baada ya Tembo hao kuonekana katika kijiji hicho wakazi wote kijijini hapo walipata hofu na wengi wao kujifungia ndani huku wachache wao wakiutumia mwanya huo kuwapiga picha Tembo hao kitu ambacho kiliwaweka katika hatari kubwa.
Mmoja wa Wananchi hao alipokuwa katika harakati za kupiga picha hizo alifukuzwa na Tembo na alipomkaribia alimfunika tembo huyo usoni kwa koti alilokuwa amelivaa hali iliyopelekea tembo huyo kupoteza mwelekeo na kuweza kuokoka kuuawa na Tembo huyo.
Diwani wa kata hiyo Egid Ngomeni alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo za kijiji hicho kuvamiwa na tembo naye alitoa taarifa halmashauri ya wilaya na Poli la hakiba la Lwafi na baada ya muda askari wanyama pori wa halmashauri na wale wa hifadhi ya pori la akiba la Lwafi walifika eneo la tukio.
Alisema kuwa askari hao walifanikiwa kuwaswaga Tembo hao na kuwarudisha katika pori la Lwafi huku ikiwa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa.
Kaimu mkuu wa Pori la akiba la Lwafi Ramadhan Abdul alidai kuwa mpaka sasa askari wapo kazini kuendelea kuwarudisha Tembo hao na kudai kuwa kwa sasa wanyama pori wameongezeka sana lakini huenda kuwa kijiji hicho kimesogea karibu sana na hifadhi hiyo kinyume cha sheria.
Alisema sheria ya uhifadhi wa wanyama Pori kifungu cha 74 namba 5 ya mwaka 2009 kipo wazi kabisa kwani kinawataka watu kuishi mita 500 toka katika mpaka wa hifadhi na kuwa licha ya askari hao kuendelea kuwarudisha tembo hao kwenye hifadhi pia wanatoa elimu kwa jamii juu ya sheria hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment