Monday, 5 June 2017

Sumbawanga waaswa kuenzi utamaduni

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

MKUU wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa Dkt Khalfan Haule amewaasa wazee wanaojua mila na desturi za makabila yaliyomo wilayani humo kuacha kujifichaficha badala yake wajitokeze na kuwafundisha watoto na wajukuu wao ili wawape urithi kwa kuwa mila na desturi ni lazima zirithishwe na wazee.

Aliyasema hayo katika kijiji cha Milanzi kilichopo nje kidogo ya mji wa Sumbawanga wakati akizindua kituo cha uhifadhi na utalii cha kabila  la  wafipa ambapo tasisi isiyo ya kiserikali ya Jumuia ya maendeleo ya mkoa wa Rukwa (JUMARU) inatarajiwa kujenga eneo la makumbusho  katika kijiji hicho sambamba na kutangaza rasmi kuwa kila mwaka mwezi wa 9 kutakuwa  kukifanyika maonesho ya utamaduni wa  kabila la  wafipa katika eneo hilo.

Mkuu huyo  wa wilaya alisema kuwa yapo mambo mengi ya jadi ambayo yamekuwa yakipotea kutokana na baadhi ya wazee kuyaficha ficha na kutotaka kuwaonesha watoto na wajukuu wao mwisho wa siku wanapomaliza maisha yao hapa duniani wanaondoka nayo.

Alisema kuwa jamii yoyote isiyojivunia asili yake ni jamii ya kitumwa kwani ni ukweli usiopingika kuwa kila kabila lina mila desturi na tamaduni zake ambazo zinafaa kuenziwa kwaajili ya kizazi kilichopo na kijacho.

Dkt Haule alisema kuwa ni jambo la ajabu sana kama kuna mtu wilayani humo ambaye haionei fahari asili yake kwani kila mtu anakabila na kila kabila linatamaduni zake ambazo ni nzuri na zinapaswa kuenziwa kwani ndizo zinazomtambulisha yeye na kabila jingine.

Alisema kuwa niwazi kuwa Sumbawanga kunakabila la wafipa ambao wanatamaduni zao na iwapo wazee wasipo waachia watoto na wajukuu wao basi watajikuta wanaiga tamaduni kutoka mahali kwingine  ambazo nyingine zinakinzana na tamaduni zao na hivyo kuonekana wamepotoka.

"Leo hii kuna vijana wanaishi kama wamarekani lakini wapo katika wilaya ya Sumbawanga huu ni utumwa kwani wanatukuza tamaduni  za watu wengine na kuziacha zao kitu ambacho sio sawa na hivyo kuishi kama kichekesho katika jamii"... Alisema.

Alisema kuwa nivema wazee wa kila kabila kujitahidi kuwarithisha watoto na wajukuu mila na desturi nzuri ikiwa ni pamoja na chakula, mavazi,tiba za asili na mengineyo ambayo yatakuwa mazuri na yatawafaa katika maisha kwani mila na desturi ni kitu cha kujivunia.

Kwaupande wake rais wa tasisi ya JUMARU, Hellen  Khamsini alisema kuwa makumbusho hayo yatakayojengwa yataunganishwa na fursa za utalii zilizopo mkoani humo ili watakao fika kutembelea makumbusho hayo wawe wanatumia nafasi hiyo kutembelea maeneo ya utalii mkoani humo.

Alisema kwa mataifa kama China na nchi nyingine wamekuwa wakifanya hivyo na kujikuta wanajipatia fedha nyingi kutokana na watalii wa ndani na nje wanaotembelea katika maeneo hayo na nchi kupata mapato kutokana na shughuli za utalii.

Akitoa shukrani zake kwa mgeni rasmi mtemi wa kabila dogo la  wa mambwe Kutazungwa Mambwe alisema kuwa wao wakiwa ni wazee wa mila na desturi watajitahidi kuwarithisha vijana na watoto ili waishi siku zote kwa kufuata asili yao kwani ndio msingi wa kila binadamu.

Mtemi Kutazungwa alisema kuwa kutokana na kuanzishwa kwa kituo hicho sambamba na kuunganisha na masuala ya utalii itasaidia kutangaza makabila yaliyopo mkoani Rukwa kwani fursa hiyo ilikuwa ikitafutwa kwa miaka mingi hatimae sasa imetimia.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment