Na Walter Mguluchuma
Katavi
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi imemuhukumu Mzee wa Baraza la Mahakama ya Mwanzo mjini Mpanda Anna Mlugala (59) kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kumtia hatiani kwakosa la kupokea Rushwa ya shilingi elfu 50 kutoka kwa mshitakiwa ambaye alikuwa na kesi kwenye Mahakama hiyo.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo na upande wa mashta ulioongozwa na Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU wa Mkoa wa Katavi Simon Buchwa.
Awali mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Simon Buchwa alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa Mlugala alitenda kosa hilo mei 21 mwaka 2015 katika eneo la Mtaa wa Makanyagio Manispaa ya Mpanda.
Siku hiyo mshtakiwa anadaiwa kuomba rushwa ya shilingi elfu 50 kutoka kwa Noelia Kakusu ili aweze kumsaidia katika kesi yake aliyokuwa ameshitakiwa katika Mahakama hiyo akituhumiea kuharibu mali.
Mwendesha mashitaka Buchwa alliambia Mahakama kuwa mshitakiwa alikamatwa baada ya Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa kupata taarifa za mshitakiwa kuomba Rushwa kiasi hicho cha fedha.
Alidai kuwa baada ya TAKUKURU kupata taarifa hizo ndipo walipoandaa mtego na kufanikiwa kumkamata Mzee huyo wa baraza akipokea kiasi hicho cha fedha katika eneo lilikuwa jirani na Mahakama hiyo.
Katika utetezi wake mshitakiwa ambae alikuwa na mashahidi watatu alidai kuwa fedha walizomkamata nazo hakua amepewa kama rushwa bali alikuwa amepewa ili akamnunulie vifaa vya kujifungula Noelia Kakusu ambaye alikuwa ndiyo mshtakiwa aliyempa rushwa ambae pia alikuwa ni mjamzito.
Madai hayo yalipingwa na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Buchwa kwa kile alichoeleza kuwa kitendo cha mshitakiwa Mlugala kutoka Mahakamani wakati kesi ikiwa inaendelea na kwenda nje ya Mahakama kuchukua fedha kwa Noelia ni ushahidi tosha kuwa mshitakiwa huyo alikuwa amedhamilia kuchukua rushwa hiyo ambayo alikamatwa nayo kufuatia mtego uliowekwa na TAKUKURU.
Hakimu Chiganga Ntengwa baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo na pande hizo zote mbili ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne na mshitakiwa watatu aliiambia Mahakama kuwa pasipo shaka yoyote mshitakiwa amepatikana na hatia ya kosa la kifungu cha sheria namba 15 ya kudhibiti na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 na hivyo inamuhukumu kwenda jela miaka mitatu.
Hivyo hakimu huyo alisema Mahakama imeamua kumuhukumu mzee huyo wa baraza kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya shilingi laki 5, hadi Mahakama ilikuwa imemaliza kazi zake mshitakiwa alikuwa ameshindwa kulipa faini hiyo na hivyo kwenda jela.
Mwisho
No comments:
Post a Comment