Thursday, 8 June 2017

Mmoja afariki dunia kwa homa inayodhaniwa kuwa ni uti wa mgongo Sumbawanga

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

SERIKALI wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa imetoa tahadhari kwa wakazi wa wilaya hiyo kutokana na kuwepo kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni homa ya  uti wa mgongo.

Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Khalfan Haule ametoa tahadhari hiyo jana kupitia vyombo vya habari ambapo alisema kuwa tayari kumeripotiwa  kuwepo kwa homa inayodhaniwa kuwa ni ya ugonjwa wa uti wa mgongo kwenye kijiji cha Tentula na Kianda kata ya ikozi Sumbawanga vijijini.

Alisema kuwa mpaka hivi sasa watu watatu wameugua na mmoja amekwisha fariki dunia kwa ugonjwa huo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema dalili za ugonjwa huo ni mtu kupata homa kali, maumivu ya kichwa na shingo kukakamaa.

Alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa ugonjwa  huo wakazi wa wilaya hiyo wanashauriwa  kuishi kwenye nyumba zenye madirisha yanayoingiza hewa ya kutosha kwani ugonjwa  huo ni hatari  kwakua unaenea kwa njia ya hewa.

Aidha alisema kuwa tayari idara ya afya wilayani humo imekwisha jipanga katika kuwahudumia wagonjwa wa ugonjwa huo pindi watakapo tokea na alitoa tahadhari iwapo mtu yeyote atakayepata dalili hizo afike hospitali mara moja kwaajili ya matibabu.

Hata hivyo baada ya rukwakwanza.blogspot.com kuwasiliana na kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Emmanuel Mtika alisema kuwa kunataarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo lakini ametuma timu ya wataalamu wa afya ili wafanye uchunguzi wa taarifa hizo katika vijiji hivyo.

Alisema kuwa kwa upande wa wagonjwa waliolazwa nao wanaendelea na matibabu na vipimo bado havijatolewa ili kuthibitisha, lakini alitoa wito kwa wanachi kuchukua tahadhari katika kuepuka ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine.

Mganga mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alisema kuwa pia wamekwisha jipanga tayari iwapo itathibitika kuwa ni ugonjwa huo ili wagonjwa waweze kutibiwa na kukabiliana ipasavyo na ugonjwa huo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment