Katavi
JESHI la polisi mkoani Katavi limetoa onyo kwa baadhi ya madereva wanaotumia vilevi kupita kiasi na matokeo kuendesha vyombo vya usafiri kwa mwendo kasi na hata kusababisha ajali kwa kisingizio kuwa wanasherehekea sikukuu.
Kaimu Kamanda wa polisi mkoani humo Benedict Mapujilo alitoa onyo hilo ofisini kwake wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusiana na namna lilivyojipanga katika kuhakikisha wakazi wa mkoa huo wanasherehekea sikukuu ya Idd kwa amani pasipo vurugu zozote.
Alisema kuwa wapo baadhi ya watu wanaoendesha vyombo vya usafiri huku wakiwa wamelewa sana na matokeo yake kuendesha kwa mwendokasi na kuhatarisha usalama wao, wa vyombo hivyo na hata watu wengine kwa kisingizio kuwa wanasherehekea sikukuu.
Kaimu Kamanda huyo aliwaonya kwa namna ya pekee waendesha boda boda ambao wakati mwingine wanakuwa kero mkoani humo kwa kuendesha piki piki zao kwa mwendo kasi bila kuheshimu sheria za barabarani hali ambayo ni hatari kwao na kwa watu wengine pia.
Alisema kuwa polisi watakuwepo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo katika kuhakikisha wanakabiliana na watu wa aina hiyo kwani hawatawaacha waendeshe vyombo vyao vya usafiri wanavyotaka kwa madai kuwa ni sikukuu.
Hata hivyo alitoa wito kwa wazazi mkoani humo kuwa makini na watoto wao wakati wanasherehekea sikukuu ya Idd kwani Mara nyingi watoto wamekuwa ni wahanga wakubwa wa matukio ya ajali katika siku za sikukuu kitu ambacho kinaweza kuzuilika iwapo watakua makini.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Katavi meja jenenali mstaafu Rafael Muhuga alitumia fursa hiyo kuwatakia kheri waisilamu wote pamoja na wakazi wote wa mkoa wa Katavi sikukuu njema huku akiwaasa kusherehekea kwa amani pasipo kutumia vilevi na waheshimu sheria za nchi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment