Na Gurian Adolf
Kalambo
MTOTO Lina Protas(5) amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu uliolipuka katika kijiji na kata ya Samazi Mwambao wa ziwa Tanganyika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa huku wengine 16 wakiwa wamelazwa kwenye zahanati ya kijiji hicho.
Akizungumza na gazeti hili ofisni kwake afisa tarafa ya Kasanga wilayani humo Peter Mankambila alisema kuwa chanzo cha ugonjwa huo kimetokana na wavuvi waliokuwa wametokea katika kijiji cha Mpasa kilichopo wilaya ya jirani ya Nkasi, ambao walifika kijijini hapo kwa shughuri za uvuvi na kuwambukiza wengine.
Amesema ugonjwa huo uligundulika Juni 16,2017 na kuwa mpaka sasa watu 16 wamelazwa kwenye zahanati ya kijiji hicho kwa matibabu zaidi.
Kwa upande wake Afisa afya wa wilaya hiyo Andondile Mwakilima ambaye licha ya kukiri kuwepo kwa ugonjwa huo alisema kuwa mpaka sasa watu wanane wameruhusiwa kurudi nyumbani huku wengine 8 zaidi wakiendelea kupatiwa matibabu zaidi na kuwa mpaka sasa wanaendelea kuhamasisha jamii kuchimba vyoo vya kudumu kwa lengo la kujiepusha na ugonjwa huo.
Akitoa hamasa katika suala mzima la kujikinga na mgonjwa huo Mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura aliwasihi wakazi wa mwambao wa ziwa hilo kutumia maji safi na salama kwa lengo la kujiepusha na ugonjwa huo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment