Na Gurian Adolf
Sumbawanga
HALMASHAURI ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imewang'oa walimu wakuu ambao hawana sifa za kuanzia stashahada(diploma) na kuendelea katika nafasi zao na kuwapa wenye sifa hizo za elimu ili kutekeleza Sera ya elimu na waraka wa serikaki kuu wa mwaka 2014 na maelekezo kutoka wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI) ikiwa ni mkakati wa kuboresha kiwango cha elimu katika shule za msingi katika Manispaa hiyo.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hamidi Njovu alisema jana katika kikao maalumu cha kazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo kuwa imemlazimu kuwaondoa walimu wote kwenye nafasi za ualimu wakuu wale wote ambao ni walimu wa daraja la IIIA na kuwaweka wenye elimu ya kuanzia stashahada na kuendelea kwakua ndivyo sera ya elimu na waraka wa mwaka 2014 unavyo elekeza.
Alisema kuwa kufuatia kuondolewa huko jumla ya walimu 25 wenye sifa ya kuanzia stashahada na kuendelea wameteuliwa kushika nyadhifa hizo na nimatumaini yake kuwa watasimamia taaluma, na kuongoza shule hizo kwa weledi mkubwa na hivyo matokeo chanya yatapatikana kutokana na mabadiriko hayo.
Mkurugenzi huyo aliwataka walimu hao wateule kukaa katika vituo vya kazi muda wote licha ya kuwa shule za Manispaa hiyo zinakabiliwa na changamoto ya ukusefu wa nyumba za walimu za kutosha na zenye hadhi lakini isiwe kigezo cha kuwavunja moyo na kuishi mbali na vituo vya Kazi kwani watambue kuwa wanadhamana kubwa ya kuhakikisha wanaleta mabadiriko makubwa na si kuwa wanyonge na kukubali changamoto ziwaangushe katika matarajio yao.
Kwaupande wake kaimu Afisa Elimu wa shule za msingi katika Manispaa hiyo, Richard Samson alisema kuwa uteuzi kwa walimu hao 25 umezingatia utendaji kazi na kigezo cha taaluma hivyo wanajukumu kubwa la kuleta mabadiriko katika shule hizo iwe tofauti na hapo awali ambapo ni mategemeo yake kuwa ufaulu utapanda kutoka kiwango cha asilimia 77.7 cha mwaka jana.
Akisema kuwa Katika mchakato wa walimu 90 wenye sifa za astashada,shahada na uzamili waliteuliwa walimu 12 wenye astashada,12 wenya shahada na mmoja wenye cheti cha uzamili ndio waliopata nafasi za kuwa walimu wa kuu katika shule 25 ambazo watapangiwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Sumbawanga Huruma Kilingo alitoa wito katika kufanya michakato mbalimbali ya kuwapandisha hatua walimu na waepuke rushwa ya aina yoyote kwani inaweza kuua kabisa elimu katika halmashauri hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment