Gurian Adolf
Katavi
Mahakama ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi, imemuhukumu kwenda jela miaka 23 Mkazi wa kijiji cha Kalovye, Osward Mpalasinge (26) baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo cheti cha kidato cha nne.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Teotimus Swai baada ya mtuhumiwa kukiri kosa mahakamani.
Awali, Mwendesha Mashtaka mkaguzi wa Polisi, Baraka Hongoli alisema kuwa mshitakiwa alitenda makosa ya kuvunja na kuiba mei 25 mwaka huu nyakati za saa mbili usiku nyumbani kwa Veronica Crispin anayeishi kijiji cha Kalovye Inyonga.
Aliieleza Mahakama hiyo kwamba mtuhumiwa alifika nyumbani hapo kavunja kisha kuiba nguo zenye thamani ya Sh 110,000 na cheti cha kidato cha nne cha Henreth Edward Kalamu kilichotolewa na baraza la Mitihani (NECTA) mwaka 2015.
Kabla ya kupewa adhabu hiyo mtuhumiwa alipewa nafasi ya utetezi ambapo aliiomba mahakama impatie muda ili aweze kwenda Dar es salaam kumtafutia mtu huyo cheti kingine.
Mwendesha Mashitaka Hongoli aliitaka mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa kuwa wizi wa aina hiyo ndio umesababisha usumbufu na watu kupoteza ajira zao serikalini na maeneo mengine pindi uhakiki wa vyeti unapofanyika.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Swai alisema pasipo shaka mtuhumiwa amekutwa na hatia hivyo anahukumiwa kwenda jela 23 kwa kuzingatia vifungu vya sheria namba 294 (1) (2) ya kosa la kuvunja na kifungu 265.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment