Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MKUU wa mkoa wa Rukwa Zelote Steven amewaonya wakazi waishio mwambao mwa ziwa Tanganyika mkoani humo kuacha kukimbilia tiba za jadi pindi wauguapo badala yake waende hospitali ili waweze kutibiwa kitaalamu magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kipindu pindu ulioibuka katika kijiji cha Samazi wilayani Kalambo mkoani humo.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samazi wilayani Kalambo mkoani humo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo ni baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kutowapeleka wagonjwa hospitali na kuwakimbizia kwa waganga wa jadi hali inayosababisha kutopata matibabu sahihi.
Alisema kuwa matibabu yanayofanyika katika hospitali ni ya kitaalamu na yanafanyiwa tafiti na hufanyika bila kukisia tofauti na kwa waganga wa jadi ambao wamekuwa wakitoa tiba zao kwa kukisia kwakua hawatumii vifaa ambavyo vinauwezo wa kuona wadudu wanaosababisha ugonjwa husika.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa katika nchi hii mtu akiugua kipindupindu na akitibiwa na kupona sheria inamtaka kufikishwa mahakamani kutokana na kitendo hicho cha kuugua ugonjwa huo kwani sababu kubwa ni kukiuka taratibu na sheria za usafi.
Alisema kuwa wale wote waliougua na kupona kipindupindu katika kijiji cha Samazi wajiandae wakati wowote serikali itakapoona inafaa inaweza kuwafikisha mahakamani kwakuwa sheria inaruhusu hilo.
"Wakazi wa kijiji cha Samazi mliougua kipindupindu na kupona kaeni chonjo,wakati wowote kuanzia sasa mnaweza kufikishwa mahakamani kutokana na kuugua kipindupindu kwakua sheria inataka hivyo,na katika hili serikali ya mkoa haina mzaha kutokana na ninyi kutofuata taratibu za afya ikiwemo ni pamoja na kuchemsha maji ya kunywa"..... Alisema
Alisema kuwa ili kukabiliana na ugonjwa huo ni lazima kila mwana kijiji hicho afuate maelekezo ya wataalamu wa afya kwakua wapo na wanatoa elimu kila siku ili kukabiliana na ugonjwa huo ambao tayari umekwisha gharimu maisha ya mtu mmoja.
Naye mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Bonifasi Kasululu alisema kuwa mpaka kufikia Jana zaidi ya watu 20 wamekwisha ugua ugonjwa huo, na wataalamu wa afya wapo katika kijiji hicho kwaajili ya kutibu watu wanaougua na kutoa elimu ni namna gani ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema kuwa jitihada zinafanyika mpaka sasa ni mtoto mwenye miaka mitano ndiyo aliyefariki dunia kwa ugonjwa huo lakini siyo sababu ya kubweteka na kuona sio tishio kwani uzembe ukifanyika unaweza kuua watu wengi zaidi hivyo basi ni jukumu la kila mtu kuchukua tahadhari asiugue ugonjwa huo.
Kwa upande wake Lilian Sichilima mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni kutokuwa na huduma ya maji safi na salama,kwani wananchi wengi wa ziwani wanategemea maji hayo kwa kila kitu, ikiwemo ni pamoja na kufua,kupika,kuogelea na baadhi yao hata kunywa bila kuyachemsha ndiyo sababu kubwa inayosababisha ugonjwa huo kuota mizizi katika kijiji hicho.
Aliiomba serikali pamoja na kutoa elimu lakini pia suala muhimu ni kuwapelekea huduma za mabomba ili maji watakayokuwa wakitumia yawe tofauti na yale ya ziwani moja kwa moja na yatoke katika chanzo kingine na hata kama yakiwa ni ya ziwani basi yatengwe kutoka ziwani na kuwekwa kwenye eneo jingine na yawe yanatibiwa ili kuua vimelea vya maradhi yanayoweza kuwadhuru tofauti na hivyo ugonjwa huo utakua unajirudia Mara kwa Mara.
Mwisho
No comments:
Post a Comment