Nkasi
WATOTO waliougua ugonjwa wa ngozi na kutengwa katika kijiji
cha Nkata kata ya Kate wilayani Nkasi afya
zao zimeendelea kuimarika kutokana na matibabu wanayoyapata kutoka kwa
mganga wa magonjwa ya ngozi katika kituo cha afya cha Nkomolo wilayani Nkasi.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Nkasi Julius
Mseleche Kaondo alionyesha kufurahishwa na maendeleo ya watoto hao baada
ya kuwatembelea jana na kuweza kujionea maendeleo ya kiafya ya watoto hao toka
waanze kutibiwa katika hospitali hiyo.
Akizungumza katika kituo hicho cha afya Mkurugenzi huyo
alimtaka Daktari huyo kufanya awezalo ili kuweza kuwarejesha wagonjwa hao
katika hali yao ya kawaida hasa kutokana na jinsi watoto hao walivyoathirika na
ugonjwa huo wa ngozi.
Alisema kuwa halmashauri itagharamia gharama zote za
matibabu na chakula katika kipindi chote cha matibabu kwa watoto hivyo kutaka
umakini mkubwa wakati wa kutoa huduma kwa watoto hao.
Mganga wa magonjwa ya ngozi anayewahudumia watoto hao Hillary
Daukajambonye alimweleza mkurugenzi mtendaji huyo kuwa ameugundua ugonjwa unawatesa
watoto hao ambao umedumu kwa muda wa miaka sita bila ya matibabu na kuwa huenda
wakapona ndani ya wiki moja hasa ni kutokana na kuwepo kwa dawa za kuwatibu
watoto hao.
Alisema ugonjwa huo unatibika na kilichobaki sasa kwa watoto
hao ni suala zima la lishe na inaonekana mazingira wanayoishi lishe ni duni na
kuwa vile halmashauri itatoa fedha itawasaidia watoto hao kupata lishe na
mavazi ili watoto hao waweze kuwa na nguo za kubadilisha kila wakati ili kuweza
kukabiliana na wadudu wanaosababisha ugonjwa huo .
Baba mzazi wa watoto hao Martin Kazumba aliishukuru
serikali kutokana na uamuzi wao wa kuichukua familia yake na kuanza kuitibu kwani
ugonjwa huo umeitesa familia yake kwa kipindi cha miaka sita na kutokana na
uduni wa maisha alishindwa kutafuta tiba ya ugonjwa huo katika familia yake
Watoto hao ambao ni Petro na Lucas Kazumba walipozungumza na
mwandishi wa habari hizi walidai kuwa walikua wamekata tamaa ya kuishi lakini
sasa wameanza kuiona faraja baada ya kuanza matibabu.
Mkuu wa mkoa alimuagiza mganga wa hospitali ya mkoa wa Rukwa
kuhakikisha kuwa watoto hao wagonjwa wa ngozi ambao wametengwa na jamii
kutokana na ugonjwa huo kwa kipindi kirefu sasa kuhakikisha kuwa wanapata
matibabu na halmashauri ya wilaya Nkasi kuchukua hatua mara moja.
Ugonjwa wa watoto hao uliripotiwa kwenye vyombo vya habari
ambapo mkuu wa mkoa Rukwa Zellote Steven kuchukua hatua mara moja baada ya
kupata habari hizo.
mwisho
No comments:
Post a Comment