Na Gurian Adolf
Sumbawanga
JESHI
la
Polisi mkoani Rukwa, linawashikilia watu sita akiwemo mjukuu
aliyekubalichukua hongo Shilingi milioni moja na kukubali babu yake
auawe kwa
kupigwa rungu kichwani kutokana na ugomvi wa ardhi.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema jana kuwa tukio la kuuawa
kwa mzee huyo aliyefahamika kwa jina la Paul Kisiwa (72) mkazi wa kijiji
cha Ng'ongo lilitokea machi 3 nyakati za jioni kwenye kijiji cha Kifinga
Kata ya Mtowisa wilaya Sumbawanga.
Taarifa kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na Diwani wa Kata ya
Mtowisa, Edger Malinyi, zilieleza kuwa baada ya kuuawa kwa mzee huyo
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM ngazi ya kata alizikwa kinyemela
shambani kwake.
Inaelezwa kuwa
taarifa za kupotea mzee huyo zilianza kuzagaa ndipo ndugu wa marehemu,
pamoja na majirani wakishirikiana na polisi walianza kuchunguza tukio
hilo,
ambapo ilipofika machi 8 mwaka huu, watu hao walimbana mjukuu wa mzee
huyo aitwaye John Kisiwa (22) ambaye alikiri kushiriki kupanga njama za
kumuua babu yake kwa ujira wa Shilingi 1,000,000.
Diwani huyo,
alisema kijana huyo alipanga njama ya mauaji hayo na wenzake ambao
walikuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na mzee huyo ambaye awali
aliwakodisha watu hao shamba la ekari zaidi 15 kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Alisema
baadaye aliwanyang'anya shamba hilo na kuamua kulilima yeye
mwenyewe kitendo kilichowauzi watuhumiwa hao ambao walijikuta wakiingia
katika mgogoro wa kugombea eneo hilo, hali ilisababisha waandae
mipango ya kumuua mzee huyo.
Inadaiwa
kuwa siku ya tukio la mauaji hayo, watu hao walimvamia mzee huyo akiwa katika
shambani lake hilo, na kisha kumpiga na rungu kichwani ambapo alianguka na
kufariki dunia papo hapo.
Diwani Malinyi
alisema baada ya kumuua mzee huyo walichimba shimo shambani humo na kumfukia ili kupoteza
ushahidi hali iliyobainika baada ya mjukuu wake kubanwa na kueleza
ukweli hivyo polisi walifukua eneo hilo na kukuta mwili wa mzee huyo.
Kamanda Kyando aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa kuwa ni Kela Lubinza
(15), Chani Lubinza (29), Simba Lubinza (16) wote wakiwa ni ndugu wa familia moja pia
Deshi Mihambo (40) na Muli Sabini (21) ambao ni majirani wa wanafamilia hao.
Alisema
watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia
sasa mara baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment