Sunday, 15 October 2017

Waaswa kufanya mazoezi kutibu magonjwa

Na Gurian Adolf
Sumbawanga 
WANANCHI Mkoani Rukwa wameshauriwa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi kwa lengo la kuboresha afya zao sambamba na kumuenzi baba wa taifa ambaye alikuwa ni mpenda michezo.
Hayo yalisemwa  na mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelote Steven katika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere katika uwanja wa Nelson Mandela,mjini Sumbawanga.
Alisema kuwa baba wa taifa alikuwa ni mpenzi wa mchezo wa bao hivyo,alionesha kuwa anapenda michezo na alikuwa ni mfuatiliaji mkubwa wa timu ya mpira wa miguu ya taifa pindi inapocheza. 
Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na jumamosi ya pili ya mazoezi pamoja na kilele cha wiki ya vijana ambapo wananchi walijitokeza asubuhi kwaajili ya kushiriki mbio zilizoanzia ofisi ya mkuu wa mkoa kuelekea kwenye viwanja vya mpira wa miguu.
Alisema wananchi wengi siku hizi wameacha kufanya mazoezi ya viungo hali inayosababisha kunyemelewa na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo na kisukari hali inayopunguza nguvu kazi ya taifa.
Aliongeza kuwa yeye binafsi katika kuweka afya yake vizuri, huwa anatumia dakika 20 kila siku asubuhi kufanya mazoezi kabla ya kuelekea ofisini hali iliyopelekea kuoneka na afya nzuri mbali na kuwa na umri mkubwa.
“Msinione bado nipo fiti ni kwasababu ya kufanya mazoezi kila siku kwa dakika 20 kabla sijaingia ofisini, mazoezi ni faida yetu wenyewewe, sio faida ya rais, makamu wa rais wala waziri mkuu, na Katika kuona kuwa watanzania wameacha mazoezi Serikali ikaagiza kila jumamosi ya pili ya mwezi iwe ya mazoezi si kwasababu nyingine bali ni kuendelea kutunza afya zetu,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema yapo matatizo mengine ya kiafya hayahitaji dawa za hospitali zenye kemikeli bali tiba yake ni mazoezi lakini serikali inaingnia gharama kubwa ya kununua madawa wakati yangeweza kutibika kwa mazoezi.
Siku hizi hata mchaka mchaka mashuleni hakuna hali hii nihatari kwa afya ya kizazi chetu hivyo ni lazima kuwe na mkakati wa makusudi wa kuifanya jamii itambue mazoezi ni muhimu kwa afya zao, alisema.
Pia alitumia fursa hiyo kumuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa huo kuhakikisha kuwa anaweka utaratibu wa kuhakikisha kila mtumishi wa serikali anashiriki mazoezi ili kuimarisha afya na kuendeleza kulijenga taifa.
Kwa upande wake Katibu tawala mkoa wa Rukwa Bernard Makali katika kuisemea kilele cha wiki ya vijana, aliwataka vijana mkoani humo kuandika maoni juu ya fani watakazotaka zifundishwe katika chuo kipya cha ufundi VETA kinachotarajiwa kujengwa katika makao makuu ya Mkoa huo,mjini Sumbawanga.
“Katika kuhakikisha huduma mbalimbali za kiufundi zinapatika katika Mkoa wetu, hivi karibuni serikali itaanza kujenga chuo cha ufundi stadi,VETA cha kisasa, hivyo wawe tayari kutoa maoni juu ya fani ambazo wanataka zifundishwe kwenye chuo hicho kwani ni fursa yao kuamua nini wafundishwe" alisema.
Aliwasihi wazazi mkoani humo kuwasomesha watoto vyuo vya ufundi kwani ni rahisi kujiajili kuliko hivi sasa ambapo wahitimu wengi wanakaa na vyeti nyumbani wakilalamika kuwa hakuna ajira.
Mwisho 

No comments:

Post a Comment