Na Gurian Adolf
Mbeya
SERIKALI mkoani Rukwa imefanya ziara ya mafunzo katika tasisi ya Utafiti Kilimo (ARI) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) nyanda za juu kusini - Uyole, Mkoani Mbeya kwalengo la kujifunza shughuli zinazofanywa na taasisi hizo ili kunufaisha maendeleo ya mkoa huo.
Ziara hiyo iliyo wahusisha Katibu Tawala wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na makatibu tawala wao na viongozi wa vikundi vya wakulima,Wakurugenzi, maafisa kilimo na mifugo wa wilaya, pamoja na wenyeviti wa Halmashauri nne za Mkoa huo, pamoja na wataalamu wa kilimo na mifugo kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Katika ziara hiyo ya siku moja mada mbalimbali zilitolewa kuhusu aina ya mazao yanayoweza kustawi katika Mkoa wa Rukwa, wadudu wanaoweza kushambulia mazao hayo na namna ya kuwadhibiti ili kuongeza uzalishaji pamoja na utafiti wa udongo.
Aidha viongozi hao waliweza kujifunza umuhimu wa kilimo cha nyasi kwaajili ya mifugo, ufugaji bora kwaajili ya viwanda vya mazao ya mifugo, magonjwa mbalimbali ya mifugo na namna ya kukabiliana nayo
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelote Steven alisema kuwa kwa miongo Mingi Mkoa wa Rukwa umekuwa katika mikoa inayoongoza kwa kilimo lakini haikuwahi kuwa namba moja hivyo ziara hiyo ndio mwanzo wa kuiendea Rukwa mpya yenye kuzalisha mazao yenye tija kwa wakulima, mkoa na taifa kwa ujumla.
“Lengo la kufunga safari kutoka Rukwa hadi hapa ni kuleta mabadiliko ya Kilimo na mifugo, kupitia kilimo ndio litakuwa chimbuko la viwanda, kama wataalamu walivyosema kuwa kilimo ndio chimbuko la viwanda,tunahitaji kuboresha kilimo katika Mkoa wa Rukwa ili tuwe na viwanda vya uhakika” Alisema
Alisema kuwa ili kuwakomboa wananchi wa hali ya chini ambalo ndio lengo la rais Dk. John Pombe Magufuli hakuna budi kuimarisha kilimo na hatimae kuinuka kutoka katika uchumi wa viwanda vidogo kwenda viwanda vya kati na kutoka katika uchumi mdogo kwenda uchumi wa kati.
Kwa upande wake mratibu wa ziara hiyo Benjamin Kiwozele alimshukuru mkuu huyo wa mkoa kwa kuona umuhimu wa kuzitumia taasisi hizo kwa malengo yaliyowekwa na serikali.
Kabla ya Kumkaribisha mkuu huyo wa mkoa Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa Kilimo Tulole Bucheyeki alisema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa mkoa wa Rukwa kwa heshima kubwa waliyoionyesha kwa kufika kwenye Taasisi hiyo na kuweza kukutana na wataalamu wao kwa nia ya kuboresha uwekezaji na vipato vya wananchi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment