Thursday, 19 October 2017

CWT yawanusuru walimu

Na Israel Mwaisaka
Nkasi
CHAMA Cha Walimu  Tanzania (CWT) wilayani Nkasi mkoani Rukwa kimewanusuru walimu 19 kufukuzwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu.
Akizungumza  jana kwenye mkutano mkuu wa CWT ulifanyika katika ukumbi wa Ngunga uliopo mjini Nkasi mwenyekiti wa chama hicho Selis Ndasi alisema kuwa walimu wanakabiliwa na changamoto kubwa ya utovu wa nidhamu na kuwa inabidi wabadilike na kuwa kutokana na hilo ilikua walimu 19 wafukuzwe kazi lakini walikingiwa kifua na chama hicho.
Alisema chama hicho kimechoka kuwalinda walimu wahalifu na kuwa sasa wanatakiwa wabadilike wawe na nidhamu kazini na kutomkorofisha mwajiri na watambue kuwa hivi sasa serikali ni chungu na ukifanya kosa moja unafukuzwa kazi na kuwa kama wakiendelea kuzembea wengi watafukuzwa kazi.
Alisema miongoni mwa matatizo yanayo wakabili walimu ni utoro kazini,uzembe,ulevi na kutowaheshimu waajiri wao na kuwa sheria inaeleza kuwa mwalimu asikuwepo kazini siku tano mfululizo bila taarifa adhabu yake ni kufukuzwa kazi.
Mkuu wa idara ya utumishi wa Walimu TSC  Richard Kityega alisema kuwa idara ya ualimu imekua ikikabiliwa na changamoto ya utovu wa nidhamu na kuwa hadi sasa walimu 24 wameshafukuzwa kazi kwa makosa hayo na kuwa wataendelea kuwawajibisha walimu kama hao kwa kuwafukuza kazi.
Hivyo aliwaomba wawakilishi wa chama hicho mahali pa kazi kuwasaidia wanachama wenzao ambao ni Waalimu kuwaelekeza namna wanavyostahili  kuishi kwa kufuata kanuni za utumishi wa umma na kuachana na mazoea na kuwa idara yao haimuonei mtu na hadi kufikia hatua ya kumfukuza kazi Mwalimu kuna vitu vingi wanakuwa wamejiridhisha.
”sisi wenyewe hatufurahii kitendo cha mwalimu kufukuzwa kazi lakini inapasa kufikia hatua hiyo baada ya makosa hayo kujirudia kila wakati licha ya kuonywa”alisema
Naye Afisa elimu wa shule za msingi wilayani humo Misana Kwangullah kwa upande wake alidai kuwa walimu kama watumishi wa umma wajitahidi kufuata tu kanuni za utumishi na  kuwa wale watakaoendelea kuenenda kinyume na maadili sheria zipo na sasa zinafanya kazi.
Mjumbe wa kamati tendaji ya (CWT) ngazi ya taifa Juma Saidia aliwataka wawakilishi wa CWT mahala pa kazi kuwasimamia wenzao na kuwaonya juu ya kufuata misingi ya ajira yao vinginevyo watakwisha.
Alisema lengo la kuwapo kwa Chama Cha Walimu si kutetea maovu bali ni kuwalinda dhidi ya uonevu na kusimamia uwajibikaji na kuwa sasa chama hicho hakitakuwa tayari kumtetea Mwalimu ambaye ataonyesha utovu wa nidhamu na kushindwa kuwajibika vyema mahala pake pa kazi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment