Tuesday, 10 October 2017

Ally Kessy kuwachukulia hatau watendaji wa vijiji

Na Israel Mwaisaka
Nkasi
MBUNGE wa jimbo la Nkasi kasikazini Ally Kessy ameahidi kuwachukulia hatua viongozi wa vijiji ambao wamefuja  fedha  zilizotolewa na serikali kwaajili ya kuchimba visima vya maji katika vijiji vyao kwalengo la kukomesha tabiaya kufuja fedha za umma. 
Hayo aliyasema jana kwenye mahafali ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Mashete ambapo aliahidi kuwapeleka wakaguzi wa hesabu katika vijiji hivyo na ripoti ikibainika kuwa kuna ubadhirifu  wa fedha hizo watakamatwa  na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Alisema kuwa serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 7 kwa kila kijiji chenye matizo sugu ya maji lakini mpaka sasa hakuna kijiji hata kimoja ambacho kimekamilisha mradi wa maji.
Kessy lisema kuwa serikali iliamua kupeleka fedha katika vijiji hivyo baada ya kilio cha muda mrefu cha tatizo la maji lakini mpaka sasa vijiji hivyo havina maji kwa maana kwamba hakuna mradi hata mmoja ambao umekamilika na kuwafanya wananchi kuendelea kutabika kwa ukosefu wa maji.
Mbunge huyo alisema  kuwa katika hilo hatakua na huruma hata kidogo na kuwa ikibainika kiongozi yeyote amehusika kwenye ubadhirifu wa fedha hizo hata achwa salama ni lazima atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo ya mbunge ilikuja kufuatia mkuu wa sekondari hiyo Gilbert Aloyce kumuomba mbunge Kessy kuwatatulia tatizo la maji katika shule hiyo ambayo imekuwa haina maji kwamuda mrefu. 
Hata hivyo serikali ilikwisha toa fedha tangu mwaka jana kwaajili ya kuchimba visima katika vijiji vyevye shida ya maji ikiwemo kijiji cha Mashete lakini hakuna kinachoendelea mpaka sasa ni lazima kwanza aanze kuwashughulikia viongozi hao wa vijiji ndipo aje kuliangalia tatizo la maji katika shule hiyo.
‘’Haiwezekani  fedha za serikali zikaachwa zikachezewa kiasi hicho wakati wananchi wana shida  kubwa ya maji na lazima tuionyeshe mfano kwa baadhi yao ili kuheshimu fedha za umma’’alisema Mbunge.
Pia mbunge huyo alionyesha kukerwa na mdondoko wa Wanafunzi katika shule hiyo ambapo kati ya Wanafunzi 63 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2014 lakini wanaomaliza sasa ni 15 tu ambapo  aliwataka wazazi kushirikiana na waalimu katika kuona jambo hilo halijirudii tena.
Mahafali hayo ni ya tano katika shule hiyo ambayo changamoto kubwa iliyopo ni utoro kwa Wanafunzi jambo linalohitaji tiba ya haraka.
Mwisho

No comments:

Post a Comment