Friday, 4 August 2017

Ugonjwa wa ajabu wazua hofu kwa wazazi

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
HOFU na mashaka imewakumba baadhi ya wazazi wa watoto wanaosoma katika shule ya sekondari ya Kirando wilayani Nkasi mkoani Rukwa baada ya watoto wao kuugua ugonjwa usiojulikana ambapo wanapatwa na kwikwi, kushindwa kuongea,kutetemeka na kuishiwa nguvu. 
Ugonjwa huo umekuwa ukiwapata wanafunzi wa kike ambao wanasoma kidato cha tano na sita katika shule hiyo kiasi cha kusababisha hofu kwa wazazi wa watoto hao huku wengine wakitaka kuwatorosha shuleni hapo na kuwapeleka kwa waganga wa jadi wakiamini kuwa wamerogwa. 
Gazeti hili lilipata nafasi ya kuwasiliana  na mkuu wa shule hiyo Erneo Mgina alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo ambapo alisema kuwa ugonjwa huo umekuwa ukitokea mara kwa mara na hasa umekuwa ukiwapata wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita. 
Alisema kuwa baada ya kuibuka kwa ugonjwa huo ambao ni wa ajabu amekuwa akiwapeleka wanafunzi hao katika kituo cha afya cha Kirando kwaajili ya matibabu.
Mgina alisema kuwa baada ya kupatiwa kulazwa na kupatiwa matibabu baadae wanaruhusiwa na kurudi shuleni na kuendelea na masomo yao kama kawaida licha ya kuwa baada ya muda unaibuka tena kwa wanafunzi wengine. 
Alisema kuwa kutokana na huduma za afya wanazopatiwa anaimani kuwa tatizo hilo litakwisha kwani katika kituo hicho cha afya inatolewa tiba ambayo inamaliza ugonjwa huo kwa mwanafunzi anayeonekana kuugua.
Kwaupande wake mganga mkuu mfawidhi wa kituo cha afya cha kirando Dkt Gabriel Majani alisema kuwa baada ya kufanyiwa vipimo hawakubainika kusumbuliwa na ugonjwa wowote ambao ni tishio bali ni matatizo ya Kisaikolojia. 
Alisema kuwa mpaka sasa kunawanafunzi 8 ambao hali zao sio nzuri sana lakini wanapatiwa matibabu na tayari yeye amekwisha toa taarifa kwa ngazi ya wilaya na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo zinaendelea. 
Dkt Majani alitoa wito kwa wazazi kutokuwa na imani potofu za kishirikina bali wawe wanaamini kuwa matatizo yote ya kiafya yatapatiwa matibabu katika kituo hicho cha afya na hali zao zitaendelea vizuri na wataendelea na masomo yao kama kawaida. 
Mwisho

No comments:

Post a Comment