Kalambo
WAVUVI wawili wakazi wa Kijiji cha Kilewani Tarafa ya Kasanga Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, wamekufa maji baada ya kuzama kwenye Ziwa Tanganyika wakati wakivua samaki.
Tukio hilo lilitokea julai 17 majira ya saa 8 za usiku baada ya wavuvi hao ambao ni marafiki walipoingia ziwani kwa lengo la kufanya shughuli zao za uvuvi ambapo walikuwa wamejiajiri kupitia sekta ya uvuvi.
Wavuvi hao waliofahamika kwa majina ya Ezekiel Nkambula(30) na Hamphrey Simlinga(30) wote walikufa baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia kuvulia samaki kupigwa na dhoruba na kuzama.
Ofisa Tarafa ya Kasanga, Peter Mankambila, alisema jana kuwa watu hao ambao ni marafiki waliondoka kuelekea Ziwani wakiwa na mitumbwi kwa lengo la kuvua samaki, na siku hiyo kulikuwa na upepo mkali na mawimbi makubwa.
Alisema kuwa walipoingia ziwani nyakati za usiku hawakurudi tena mpaka baada ya siku mbili ndipo ndugu na jamaa waliamua kufuatilia kutaka kujua nini kiliwakuta ndugu zao hao ambao haikuwa kawaida yao kuto rejea kijijini kwa muda mrefu licha ya kuwa walikuwa wamezoea kufanya shughuli hiyo ya uvuvi.
Alisema baada ya kufuatilia ndani ya maji kwa kuwatafuta kwa muda mrefu walifanikiwa kuona nguo wakizokuwa wamevaa zikielea kwenye maji ndipo walipo aminini kuwa watu hao wamekufa maji maana haiwezekani nguo walizokuwa wamevaa kuelea na wenyewe wakiwa wamebaki hai.
Baada ya kuzipata nguo hizo walirudi nazo kijijini kama ushuuda wa vifo vya watu hao na kulazimika kuweka msiba wakiamini kuwa ndugu zao walikuwa wamefariki dunia kwa kuzama katika ziwa Tanganyika.
Alisema kufuatia hali hiyo, walitoa taarifa polisi kufuatia tukio hilo na kujiridhisha kuwa ndugu zao hao watakuwa wamekufa maji kwakua siku hiyo ziwani kulikuwa na upepo mkali na mawimbi makubwa.
Aidha, Mankambila alisema hata hivyo, miili ya marehemu hao bado haijapatikana huku viongozi wa serikali wa kijiji na tarafa wanaendelea na jitihada za kusaka miili ya watu hao.
Mankambila alitoa wito kwa wavuvi kuchukua tahadhari kwa kutokwenda kufanya shughuli za uvuvi pindi ziwa hilo linapokuwa na dhoroba na mawimbi kwani ni hatari wanaweza kupoteza maisha kwa kuzama majini kutokana na dhoruba inayokuwa ndani ya ziwa hilo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment