Na Gurian Adolf
Katavi
ASKARI wa hifadhi za Taifa (TANAPA) wameonywa kutojihusisha na vitendo vya ujangili kwani wakibainika kufanya hivyo hatua kari zitachukuliwa dhidi yao kwakua wao ndio wanandhamana kubwa ya kulinda hifadhi hizo.
Mwenyekiti wa bodi ya Wadhamini ya TANAPA Mkuu wa Majeshi mstaafu Meja jenerali George Waitara alitoa onyo hilo jana kwa askari wa Hifadhi za Taifa wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya askari hao wapatao 153 wa kutoka Tanapa na Hifadhi ya Ngorongoro yaliofanyika katika kituo cha mafunzo Mlele Mkoani Katavi yenye lengo la kuwaandaa ki utendaji kazi wa kutoka mfumo wa sasa wa kiraia na kuwa mfumo wa Jeshi usu.
Alisema zipo taarifa za kuwepo baadhi ya askari wa hifadhi za Taifa na wa mapori ya akiba wamekuwa sio waaminifu na wamekuwa wakifanya shughuli za ujangili kwenye mapori ya akiba na kwenye hifadhi za Taifa kitu ambacho ni makosa makubwa.
Aliwataka wale wote wenye tabia hiyo waache mara moja na watakao bainika wajue kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu na kufikishwa Mahakamani bila kujali cheo wala wadhifa wa mtu kwani jukumu walilonalo ni kulinda hifadhi hizo.
Mwenyekiti huyo wa bodi ya Tanapa alifafanua kuwa kamwe huwezi kuwa wewe ni askari unae linda maliasili za nchi na huku ukiwa ni mhalifu wa maliasili za nchi yetu na hautavumiliwa.
Alisema Tanzania ilikuwa imekubwa na changamoto kubwa ya ujangili wa kutumia silaha za moto na hasa za kivita ila kutokana na mafunzo waliopata askari kwenye kituo cha Mlele ya mfumo wa jeshi usu yamesaidia sana kupunguza ujangili wa kuua wanyama kama Tembo na Faru hata hivyo sio kwamba ujangili umeisha kabisa.
Pia alisema Hifadhi za Taifa na mapori ya akiba pia yanakabiliwa na changamoto ya uingizwaji wa mifugo ndani ya hifadhi hivyo ni imani yake kuwa kupitia mafunzo yanayotolewa kwenye kituo cha Mlele askari wa hifadhi za Taifa na wa mapori ya akiba wahakikishe hifadhi zinakuwa salama kabisa .
Alieleza kuwa kazi kubwa iliyombele ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kulinda maliasili za nchi ili vizazi vijavyo vikute wanyama kama Tembo na Faru ambao wako hatarini kutoweka kutokana na ujangili.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hifadhi za Taifa Mtango Mtahiko alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuwaandaa wahitimu kwa kuwajengea utimamu wa mwili na kuwapa mbinu za kupambana na ujangili.
Pia alisema mafunzo hayo yatawaongezea ujasiri ,kujiamini na hari zaidi katika kulinda rasilimali za wanyama pori na maliasili kwa ujumla na mpaka sasa askari 830 wa Tanapa wameisha patiwa mafunzo kama hayo katika kituo cha Mlele kati ya askari 837 walipangiwa huhudhuria mafunzo hayo ya mfumo wa jeshi usu.
Mwakilishi wa Muhifadhi Mkuu wa mamlaka ya Ngorongoro Izraeli Lamon alisema Hifadhi ya Ngorongoro inakabiliwa na changamoto ya wanyama kuishi na watu ndani ya hifadhi.
Mkuu wa Hifadhi wa kituo cha Sanane Abeli Mtui alisema mafunzo hayo yatawafanya wahitimu wafanye kazi kwa uadilifu mkubwa tofauti na awali.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa mara ya 14 katika kituo cha Mlele tokea Wizara ya Maliasili na Utalii ilipotangaza kubadili mfumo wake wa utendaji kazi kwa watumishi waliochini ya Wizara hiyo kwa kutoka mfumo wa sasa wa utendaji kazi wa kiraia na kuwa jeshi usu PARAMILITARY TRANSFORMATION
Mwisho
No comments:
Post a Comment