Saturday, 15 July 2017

Wananchi wa Malangali kulipiwa huduma za Afya

Na Gurian Adolf 
Sumbawanga
MBUNGE wa jimbo  la  Sumbwanga mjini Aesh Hilaly ameahidi kuwalipia huduma ya afya ya jamii (CHF) zaidi ya kaya  150 za kata ya Malangali mjini Sumbawanga ili waweze kupata huduma za matibabu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mbunge wa Sumbawanga mjini Aesh Hilary akiwahutubia wakazi wa kata ya Malangali

Ahadi hiyo aliitoa  Jana katika kata ya Malangali mjini Sumbawanga wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za maendeleo katika jimbo  lake la  Sumbawanga mjini.
Awali akimkaribisha Hilary ili awahutubie wananchi wa kata hiyo, diwani wa viti maalumu  wa kata ya Malangali Maria Kipalashya alimueleza mbunge huyo kuwa moja kati ya changamoto zinazowakabiri wananchi wa kata hiyo ni kutokuwa na fedha za kulipa huduma za afya na hivyo kujikuta wakipata shida ya kupata matibabu kwani wakati mwingine wamekuwa wakiugua wakati hawana fedha.
Wakazi wa kata ya Malangali mjini Sumbawanga wakimsikiliza mbunge wao
Alisema kuwa wapo watu ambao wanahali  duni  zaidi ya mia moja ambao wanatamani  kuwa na huduma ya afya ya jamii lakini wanashindwa  ambapo baadhi diwani huyo aliweza kuwalipia lakini kutokana na kutomudu kuwalipia wote anamuomba mbunge huyo amsaidie kwani yeye anafursa kubwa zaidi ya kiuchumi kupitia mfuko wa jimbo na wahisani wengineo  ambao anaweza  kupata fedha na kuwalipia wananchi hao wakaingia katika huduma hiyo.
Hilary alimwambia diwani huyo afike ofisini kwake siku ya jumatatu ambapo atamkabidhi fedha kiasi cha shilingi 1,500,000 fedha ambazo zitatumika kulipia huduma ya afya ya jamii kwa kaya  zaidi ya 150 kwani kwa mpango huo kila kaya  inapaswa kulipa shilingi 10,000 na watapata huduma za matibabu kwa  watu 10 katika kaya husika kwa kipindi cha mwaka mzima.
Aidha mbunge huyo aliwaasa  wananchi za kata hiyo kuchungia shughuli za maendeleo katika kata yao bila kujali itikadi za kisasa kwani wanapaswa Ku tambua kua maendeleo hayana chama na wanafanya  kwa faida zao kwani kuvutana kwa misingi  ya kisiasa  wanajichelewesha  wao wenyewe.
Alisema kuwa mpaka hivi sasa ilani inayotekelezwa ni ya chama cha mapinduzi hivyo basi ni busara kutekeleza mipango yote ya maendeleo inayoendelea katika kata hiyo kwani kuvutana kwa kisingizio cha kisiasa  hakuna tija mwisho wa siku watakao chelewa kuendelea ni wao wenyewe na chama cha mapinduzi kipo  madarakani mpaka mwaka 2020 hivyo basi ni vizuri wakafikiri kuhusu maendeleo kwanza.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano  hivi sasa inamipango  mizuri  ya kuuboresha mji wa Sumbawanga kwa kujenga barabara, kuwapa wananchi huduma za maji safi na salama, afya na mengineyo mengi hivyo ni vizuri wakaiunga mkono bila kujali itikadi za kisiasa  ili Manispaa ya Sumbawanga isonge mbele.
Katika mkutano huo vijana wa kata hiyo walimueleza mbunge wao huyo kuhusiana na kero ya ukosefu wa ajira ambapo alitoa wito kwa watu kuwekeza viwanda ambavyo  vitatoa ajira kwa vijana wa kata hiyo ambapo itachangia kukabiliana na wimbi la  ukosefu wa ajira kwani viwanda vinaajiri watu wengi wa kudumu na vibarua ambao watajipatia kipato kupitia uwekezaji huo.
Alitoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kuwa wepesi kwenda kupata matibabu pindi wanapougua ili kata hiyo iwe na Nguvu kazi ambayo itazalisha na wawe wanaheshimu maelekezo ya wataalamu wa afya ili waishi maisha marefu  kwani bado kata inahitani nguvukazi kutoka kwao na itapatikana kwa kuheshimu taratibu za huduma za afya kula vizuri kulala vizuri na kujituma katika kufanya mazoezi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment