Monday, 31 July 2017

Manyanya aagiza wanafunzi wenye ulemavu wajengewe vyoo kwenye mabweni

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Naibu Waziri wa Elimu Mhandisi Stella Manyanya amemuagiza msimamizi wa ukarabati wa shule ya Sekondari Kantalamba kuhakikisha kuwa walemavu wanajengewa vyoo vyao ndani ya mabweni wanamolala ili kuepuka kuwaamsha wenzao usiku pindi wanapotaka kwenda kujisaidia. 
Ametoa agizo hilo jana muda mfupi baada ya kufanya ukaguzi wa ukarabati wa shule hiyo iliyopo Wilayani Sumbawanga iliyopewa Shilingi Bilioni 1.1 ikiwa ni mpango wa serikali wa kuzirudishia hadhi shule kongwe nchini huku shule hiyo ikiwa imejengwa tangu 1964 na haijawahi kufanyiwa ukarabati. 
“Lazima muhakikishe kwamba Mnakuwa na vyumba maalum kwaajili ya wanafunzi wenye ulemavu na kuwawekea miundombinu hasa kwa wale wenye  ulemavu ambao mazingira yao ni magumu Zaidi, kwa mfano mwanafunzi ana ulemavu wa miguu na anatakiwa kwenda kujisaidia hapaswi kutambaa kwenye mikojo ya wanafunzi wenziwe hii inawapelea wao kuwa katika mazingira hatarishi zaidi,” Alisema.
Mbali na agizo hilo pia Mhandisi Manyanya ametoa wiki tatu ukarabati wa shule hiyo uwe umekamilika  kwani muda waliopangiwa ulikwishamalizika huku kipaumebele kikiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo yao katika hali ya utulivu.
“Sijaridhishwa na kasi ya ukarabati huu hivyo tumewaongezea wiki tatu mhakikishe mnamaliza ili wanafunzi waendelee na masomo maana yake kama mngekuwa hamwezi kumaliza kwa wakati kwanini msingesema mapema,” Alihoji
Aidha alipokuwa anakagua bwalo la kulia chakula wanafunzi aliagiza kutanuliwa kwa bwalo hilo baada ya kuona kuwa bwalo hilo ni dogo na wanafunzi ni wengi kiasi ambacho ingewabidi wanafunzi hao kula kwa zamu ili wote waweze kulitumia bwalo hilo na kuongeza kuwa ukarabati unaofanyika ni pamoja na utanuzi wa majengo kwani ukubwa wa jengo lililopo ni wa tangu 1964 na sasa ni 2017 hivyo haliendani na mahitaji na wakati. 
Kabla ya kumaliza ziara yake shuleni hapo aliwasisitizia wanafunzi kuwa nia ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kuwa hakuna tofauti kati ya shule za serikali na shule binafsi kuanzia huduma za majengo, elimu na vifaa vya kusomea. 
Mwisho

No comments:

Post a Comment