Sumbawanga
MADIWANI wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamemtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa hiyo kuto ogopa kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji hata kuwafikisha mahakamani kwamadai kuwa wakishinda kesi halmashauri hiyo itawalipa fidia.
Akizungumza katika baraza maalumu la madiwani jana likiloketi kwa lengo la kujibu hoja za mkaguzi mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali CAG mmoja wa wajumbe wa baraza hilo Vitalis Ulaya alisema kuwa yapo baadhi ya mambo ambayo yanafanywa kwa makosa kwa makusudi kwakuwa wanajua kuwa hawawezi kufikishwa mahakamani.
Alisema kuwa utakuta katika baadhi ya malipo yanafanyika bila stakabadhi ama kutumia mashine za EFDs huku watendaji hao wakijua kuwa ni makosa lakini katika hali ambayo ni yakustaajabisha wamekuwa wakifanya hivyo.
Ulaya alisema kuwa kitendo hicho kamwe hakivumiliki kuona halmashauri hiyo inapata hati ya mashaka kwani kwa upande wa madiwani wamechoka na hawako tayari kuona watendaji wakiwaangusha.
Alisema kuwa baadhi ya vitendo vinaonesha wazi kuwa wapo watendaji ambao wapo kwaajili ya kuchuma fedha za wananchi na wamekuwa wakiishia kuonywa kwa barua bila kufikishwa katika vyombo vya sheria kitu ambacho sio sawa.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa alisema kuwa watendaji ambao wapo ndani ya uwezo wao wawachukulie hatua kwani hata wakihamishiwa sehemu nyingine watakwenda kufanya mambo ya hovyo kama hayo.
"ndugu zangu hakuna cha kuhamisha mtumishi hapa, bali kwawale ambao wapo ndani ya uwezo wetu tuwawajibishe maana hakuna halmashauri ambayo ipo tayari kupokea mtumishi wa hovyo ambaye amesababisha matatizo katika halmashauri nyingine" alisema Malisawa.
Awali mkaguzi mkazi wa ndani John Nalambwa aliwasilisha hoja 60 zenye utata ambapo hoja tatu ndizo zilizosababisha halmashauri hiyo kupata hati ya mashaka.
Alisema kuwa hoja hizo zimetokana na ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2015 hadi 2016 hivyo aliwataka madiwani pamoja na watendaji kuhakikisha kuwa suala hilo halijitojezi tena kwani si jambo jema kwa halmashauri Kupata hati yenye mashaka.
Mwisho
No comments:
Post a Comment