Na Gurian Adolf
Sumbawanga
POLISI mkoani Rukwa inawasaka watu watatu wanaodaiwa kumuua kwa kumpiga marungu Victoria Kalungwizi(67) wakimtuhumu kuwa ni mwizi wa mahindi shambani kwao.
Tukio hilo la mauaji lilitokea Julai 10 majira ya saa 11:00 jioni huko katika kijiji cha Lyapona kata ya Kaengesa, tarafa ya Mpui, wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando aliwaambia waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa wa wizi wa mahindi aliuawa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na rungu na watu watatu ambao walitekeleza mauaji hayo.
Alisema kuwa chanzo cha kufanya mauaji hayo ni kuwa walikuwa wakimtuhumu Kalungwizi kwa wizi wa mahindi ambapo marehemu alishukiwa kuwa ameiba mahindi katika shamba la Michael Mkombozi.
Mbinu waliyotumia ni kumvizia akiwa shambani anavuna mahindi katika shamba ambalo si lake na kuanza kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na na marungu hadi kumsababishia kifo papo hapo.
Kamanda Kyando alisema baada ya Watuhumiwa kutekeleza mauaji hayo walitoroka na kukimbilia kusiko julikana ambapo aliongeza kuwa juhudi za Polisi za kuwatafuta zinaendelea.
Hata hivyo kamanda huyo wa polisi aliendelea kusisitiza tabia ya wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi kwa kuwaua watuhumiwa bali wawe wanawafikisha kwenye vyombo vya sheria ili sheria ifuate mkondo wake.
Mwisho
No comments:
Post a Comment