Sumbawanga
MWANAMKE aliyefahamika kwa jina la Anna Kashamakula(40) ameuawa kwa kuchomwa kisu na mumewe wake baada ya kumhoji kuhusiana na mwanaume huyo kuchukua fedha za kulipia kodi ya nyumba wanayoishi kiasi cha shilingi 30,000 na kudaiwa kwenda kula raha na hawara yake.
Tukio likitokea jana majira ya saa 6 za usiku katika kitongoji cha Mafulala mjini Sumbawanga baada ya kuibuka mzozo baina ya wanandoa hao ambapo mke alimtuhumu mume wake kuwa amechukua fedha hizo ambazo yeye amezipata baada ya kufanya biashara ndogo ndogo na kisha kwenda kuzitumbua na hawara yake.
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa Mafulala,Christopha Kalingi alisema kuwa kabla ya mauaji hayo ulizuka mzozo baina ya wanandoa hao ambapo marehemu alikuwa akimtuhumu mumewake huyo kuwa amechukua fedha hizo na kwenda kula raha na hawara yake.
Baada ya mzozo wa muda mrefu ndipo mtuhumiwa huyo alipokasirika na kwenda kwenye chumba cha watoto wao na kuwafungia mlango kwa nje na kisha kuamua kumpiga mke wake na kumchoma kisu tumboni na kumsababishia jeraha kubwa lililosababisha kuvuja kwa damu nyingi.
Baada ya kutenda tendo hilo mtuhumiwa alikimbia na kwenda kujificha porini, ambapo baada ya tukio hilo watoto wa wanandoa hao walipiga kelele za kuomba msaada ndipo majirani walipofika ili kumkimbiza mwanamke huyo hospitali kwaajili ya matibabu.
Mwenyekiti Kalingi alisema kuwa kutokana na kuwa tukio hilo lilitendeka nyakati za usiku na ilikuwa tabu kupata usafiri wa kumuwaisha hospitali majeruhi kitendo kilichosababisha avuje damu nyingi kwenye jeraha lake na kufariki dunia wakati wakiwa njiani wakimuwahisha hospitali kwaajili ya matibabu.
Asubuhi polisi wakianza msako ndipo walipofanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa amejificha porini na anashikiliwa na polisi ambapo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaonya wakazi wa mkoa huo kuacha tabia ya kunywa pombe kupita kiasi pamoja na uvutaji wa bangi kwani vitu hivyo vimekuwa vikiwasababisha wakazi wa mkoa huo kutenda matukio ya uhalifu mara kwa mara na kuwasihi kushirikisha ndugu na jamaa katika kutatua matatizo ya kifamilia kuliko kujichukulia sheria mkononi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment