Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAKULIMA
mkoani Rukwa wameiomba serikali ianze mikakati ya kuwatafutia soko la
uhakika la mazao yao kutokana na mazao ya chakula kuzidi kuporomoka
bei baada ya mavuno kuongezeka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Ombi
hilo limetolewa kwa nyakati tofauti na wakulima wa mkoa huo wakati
wakizungumza na gazeti hili na kusema kuwa zao la mahindi limeshuka bei
kwa kasi kubwa kutoka shilingi 110,000 wiki mbili zilizopita hadi
kufikia shilingi elfu 50,000 kwa kipimo cha gunia lenye uzito wa
kilogramu 100 hivi sasa.
Wakizungumzia
kushuka huko kwa bei wakulima hao wamesema kuwa kutokana na kushuka
kwa kasi kubwa kwa zao la mahindi ambalo ndiyo tegemeo kwa wakazi wa
mkoa huo ambapo zaidi ya asilimia 90 wamejiajiri katika kilimo hususani
cha mahindi huenda wakaendelea kuto ona tija wanayoipata kutokana na
kushuka huko kwa bei ya mahindi wakilinganisha na gharama za
uzalishaji.
Mmoja wa
wakulima hao Peter Kayanda alisema kuwa serikali haina budi kuwasaidia
wakulima wa mkoa huo kupata soko la uhakika kutokana na kuwazaia
wasiuze nje ya nchi ambako soko lake huwa ni zuri tofauti na kuuza
humu nchini kwani bei wanayouzia huwa haiwapi faida.
Alisema
kuwa ni ukweli usiopingika kuwa kadiri siku zinavyozidi kuongezeka
ndivyo ambavyo wakulima wanazidi kukata tamaa ya kulima kutokana na
kutoona faida ya kilimo wanacholima na maisha yanazidi kuwa magumu kwao
na mpaka hivi sasa waliobaki wanalima ni wazee lakini vijana
wanaofikiri katika kupata faida kubwa wamekwisha acha siku nyingi
kutokana na kutoona faida kwa kukosa soko.
Naye
Maria Kalemela alisema kuwa kila siku zinavyoongezeka ndivyo wakulima
wanavyozidi kuwa na maisha magumu kutokana na kupanda kwa bei ya
pembejeo, gharama za uzalishaji na ukosefu wa soko la mazao na hivyo
hawaoni ahueni wanayopata katika kilimo na kujikuta wakikata tamaa
kuendelea kulima.
Alisema
kuwa licha ya kwamba serikali imekuwa ikinunua mahindi kwa bei ndogo
ya shilingi 500 kwa kilo lakini bado ni wakulima wachache ndio wanaouza
na mahindi mengi wanabaki nayo kwakua serikali haina uwezo wa
kuyanunua yote na kuishia kupika pombe kutokana na kukosa kwa kuyauza
au kupecha ndani kutokana na kutokuwa na soko la uhakika hapa nchini.
Kalemela
alisema kuwa wanaonufaika kwa kiasi kidogo ni wafanyabiashara ambao
wananunua mahindi yao kwa bei ya kuwalalia tena kwa vipimo wanavyotaka
wao na kujaza lumbesa na kutafuta soko na kuzidi kumkandamiza mkulima
ambaye anazalisha kwa gharama kubwa na kuishia kupata hasara.
Alisema
kuwa huenda siku zijazo wakulima nao wakachoka na kuamua kuacha kulima
kutokana na hasara wanayopata wakafikilia kufanya shughuli nyingine
kutokana na kuchoshwa na changamoto wanazokutananazo katika kilimo
kwani nao wanahitaji maisha mazuri na waliamini wangeyapata kupitia
kilimo lakini imekuwa ni tofauti.
Hata
hivyo wakulima hao waliendelea kuiomba serikali kuwakomboa kwa
kuwatafutia soko la uhakika ambalo litawasaidia kuuza mazao yao ili
wapate faida na waweze kukidhi mahitaji ya maisha yao pamoja na
kuzihudumia familia zao ambazo nazo zinazidi kutopea katika lindi la
umasikini kutokana na wazazi wao kushindwa kuyamudu maisha kutokana na
kutopata tija katika kilimo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment