Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Mwanamke aitwaye Elizabeth Kalinga(36), Aliuawa Juni 14,majira ya usiku wa saa 3:45 katika kijiji cha Sakalilo tarafa ya Kipeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya kichwani na taya la kushoto na watu ambao hawajafamika.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alisema kuwa chanzo cha mauaji bado kinachunguzwa.
Alisema kuwa kabla ya mauaji hayo
watuhumiwa walimkuta Kalinga akiwa nje ya nyumba yake na kumuuliza kama mtoto wake ambaye ni Justine Kalinga yupo na alipowauliza sababu za kumtafuta ndipo walipofyatua risasi moja juu na kumpiga na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni panga.
Katika tukio jingine likilotokea siku hiyo hiyo majira ya saa 01:45 za jioni huko katika kijiji cha Mpui, kata na tarafa ya Mpui, wilayani humo watu wawili ambao mmoja alijulikana kwa jina moja la Rasi, waliuawa kwa kushambuliwa kwa vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao na kisha kuchomwa moto na wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira kali.
Chanzo cha tukio hilo ni wizi wa mifugo ambapo walihisiwa kuwa ni wezi kwani walikutwa wanaswaga ng’ombe wawili ambao walihisiwa kuwa watakuwa wameiba na kuanza kuwashambulia na kisha kuwachoma moto.
Alisema kuwa watuhumiwa wote waliokamatwa wanashikiliwa na polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Hata hivyo Kamanda huyo wa polisi alitoa wito kwa wananchi mkoani humo kuacha tabia mbaya ya kujichukulia sheria mikononi kwa kuwapiga na kuwaua wahalifu mbalimbali kwani ni kosa kisheria badala yake wawe wanawafikisha katika vyombo vya sheria ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment