Tuesday, 6 June 2017

Milepa Waaswa kutunza Mazingira

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

WAKAZI wa kijiji cha Milepa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wameshauriwa kutojisahau nakufurahia ushindi wa kijiji chao kushika nafasi ya tano kitaifa katika mashindano ya uhifadhi wa mazingira na kusahau kuendelea kuyatunza mazingira ya kijiji hicho na wakajikuta kijiji chao kikigeuka jangwa kutokana na uharibifu wa mazingira.

Ushauri  huo umetolewa Jana na diwani wa kata ya Milepa Scolastica Malocha wakati akihutibia wananchi wa kijiji hicho katika maadhimisho ya kilele cha sherehe za Mazingira yaliyofanyika katika kijiji cha Milepa wilayani humo.

Malocha alisema kuwa kijiji hicho kimefanikiwa kushika  nafasi ya tano  kitaifa baada ya kushindanishwa vijiji  zaidi ya 150 hapa nchini na kikafanikiwa kushika  nafasi hiyo kitaifa kutokana na wananchi wake kutoharibu Mazingira na kujua umuhimu wa kuendelea kuyatunza.

Alisema kijiji hicho kina kila sababu ya kuwa miongoni mwa vijiji  bora vya mfano katika uhifadhi wa Mazingira hapa nchini kwani kina mazingira  mazuri ikiwemo ni pamoja na miti, nyasi na maji  ya tiririkayo kutoka milimani na hivyo kukifanya kiwe  cha kijani katika kipindi cha mwaka mzima, na hii haitokei bahati mbaya ni kutokana na wananchi wa kijiji hicho kuheshimu sheria za utunzaji wa Mazingira.

Diwani huyo alisema kuwa iwapo jitihada zitaendele kwa kila mwananchi ipo  siku kikafanikiwa kushika  nafasi ya kwanza kitaifa kwakua anaamini  wananchi wa kijiji cha Milepa ni wasikivu na wanapenda Mazingira na hivyo wataendelea  kuwekeza jitihada kubwa katika kupanda  miti na kutunza Mazingira mazuri yaliyopo sambamba na kutolima katika vyanzo vya maji. 

Alisema kuwa bonde  la  ziwa Rukwa linafaa sana katika kilimo cha mahindi na mpunga hivyo basi wananchi hawanabudi kuendelea kuhifadhi Mazingira ili kuwe  na mvua za uhakika zitakazo wawezeshe kufanya shughuli za kilimo bila kuwa na hofu ya ukame utakao tokana na uharibifu wa Mazingira.

Malocha pia aliwasihi wafugaji waliopo katika bonde  hilo kuwa na mifugo michache ambayo itaendana na uwezo wa kuihufumia pasipo kuharibu Mazingira kwani nalo hilo limekuwa  changamoto kubwa iwapo jitihada za kuwaelimisha wafugaji ni namna  gani ya kufuga kwa kuzingatia eneo la  malisho vinginevyo changamoto hiyo inaweza kuwa ni kikwazo cha uhifadhi wa Mazingira.

Hata hivyo aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kutunukiwa cheti maalumu na taifa  kwa kushika  nafasi hiyo pamoja na zawadi ya shilingi laki  moja na kusema kuwa hiyo iwe ni chachu ya kuwafanya  wananchi wa kijiji hicho na wilaya ya Sumbawanga kwa ujumla kuongeza jitihada katika uhifadhi wa Mazingira.

Naye kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Habona Kwileluya aliwaambia wananchi wa wilaya hiyo kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya Mazingira kitaifa mwaka huu inasema kuwa hifadhi  ya Mazingira muhimili kwa Tanzania ya viwanda na iwapo itatekeleza ipasavyo basi viwanda havitakuwa tishio katika mazingira.

Alisema kuwa miongoni mwa changamoto kubwa katika uharibifu wa Mazingira ni viwanda na serikali ya awamu ya tano  hivi sasa imejikita katika kuhimiza uchumi wa viwanda hivyo basi ni vizuri kuhifadhi Mazingira ili viwanda visije kuwa ni tishio kwa Mazingira na viumbe hai  wengine waishio wilayani humo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment