Peti Siyame
Sumbawanga
MKAZI wa kijiji cha Tunyi kata ya Mabwe Nkoswe wilaya ya kalambo mkoani Rukwa Matipa Sizunzu (20) aliyepotea tangu sepetembea 2016 katika mazingira ya kutatanisha kisha ndugu zake kuweka msiba wakiamini kuwa ndugu yao amefariki dunia amepatikana akichunga ng’ombe za mmoja wa wafugaji kijijini hapo.
Tukio hilo la kushangaza limetokea kijijini hapo baada ya kijana huyo kupatikana akichunga ng’ombe wa Juma Maeka na kupelekea wananchi kukumbwa na taharuki baada ya mfugaji huyo kugoma kumrejesha kijana huyo kwa ndugu zake akitaka kulipwa kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000=/) ambazo alizitoa wakati wa msiba mara baada ya kijana huyo kudaiwa
kufariki dunia kwa kuliwa na fisi.
Diwani wa kata hiyo Julias Kanowaliwa Siwale, alisema kabla ya kupotea kijana huyo alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng’ombe kwa mfugaji huyo ,ambapo baada ya kupotea kwake alimuakutoa fedha kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya kusaidia msibani.
Alisema baada ya msiba kumalizika kila mtu aliamini kuwa kijana huyo alikuwa amefariki dunia na kuja kushangaa baada ya ndugu na kijana huyo kumkuta kijana wao akichunga ng’ombe wa mfugaji huyo katika moja ya mbuga iliopo kijijini hapo.
Alisema baada ya kumtaka warudi nae nyumbani mfugaji huyo aliwakatalia akitaka kulipwa fedha ambazo alitoa wakati wa msiba na kupelekea kujitokeza kwa malumbano baina yao.
Alisema baada ya malumbano kuwa makubwa ikawalazimu kama uongozi wa kata kuingilia kati na kuweka kikao na kumwamuru mfugaji huyo kumrejesha kijana huyo kwa ndugu zake sambambana kumpiga faini mfugaji huyo kiasi cha shilingi laki moja kama fidia kwa ndugu wa kijana huyo.
Mtendaji wa kata hiyo Oswald Kalindo, alisema awali kila mtu alikuwa na matumaini kuwa kijana huyo alikuwa amefariki dunia kwani walimtafuta kila mahali kijijini humo na maeneo ya jirani kwamuda mrefu bila mafanikio na kuamua kuweka msiba wakiamini kuwa alikuwa ameliwa na fisi kutokana na kuwa na fisi wengi katika kijiji hicho.
Alisema kupatikana kwa kijana huyo kumeleta faraja kwa wakazi wa kata hiyo kutokana na kwamba kila mmoja alikuwa na wasiwasi juu ya kupotea kwake.
mwisho
No comments:
Post a Comment