Israel Mwaisaka
Nkasi
MKAZI mmoja wa kijiji cha Mwenge kata ya Kate wilayani Nkasi mkoani
Rukwa Joseph Songaleli (56) amefariki dunia baada ya kuuwawa kinyama na
watu wasiofahamika
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Mwenyekiti wa kijiji hicho Medadi kitinsi alisema kuwa marehemu huyo
alivamiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia juzi majira ya saa sita usiku
ambapo watu watano wenye silaha za jadi waliuvunja mlango wa nyumba ya
marehemu kwa kutumia jiwe kubwa aina ya Fatuma ambapo waliingia na
kuanza kumshambulia mtu huyo.
Alisema awali mke wa marehemu baada ya mlango kuvunjwa alitokea dirishani na kukimbia na ndipo wauaji hao walipopata nafasi ya kumkamata mume wake na kuanza kumshambulia kwa silaha hizo za jadi ikiwemo marungu na mapanga.
Alidai kuwa kulitokea mapambano makali kati yao ambapo marehemu alijitahidi kujiokoa lakini alizidiwa nguvu na akaamuliwa alale kifudifudi na ndipo alipoanza kukatwa mapanga kichwani hadi walipo muua.
Mwenyekiti huyo wa kijiji amedai kuwa mauaji hayo chanzo chake kikuu ni imani za kishirikina ambapo inasemekana marehemu aliingia mgogoro na mmoja wa ndugu zake akidai kuwa marehemu alikua akimroga .
habari za Kipolisi zinadai kuwa mpaka sasa wanamshikilia mtu mmoja kuhusika na tukio hilo na kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ili kuweza kuwakamata wale wote waliohusika katika tukio hilo.
Mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda amesikitishwa na mauaji hayo ambayo chanzo chake kikuu ni imani za kishirikina na kuwa serikali inachokifanya ni kuhakikisha wale waliohusika wanakamatwa na sasa wataanza kupita kila kijiji na kuanza kuielimisha jamii juu ya kuachana na imani hizo potofu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment