Na Gurian Adolf
Katavi
BARAZA la madiwani la Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi limeshauri itolewe elimu kwa wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi katika manispaa hiyo ili wajiepushe na tabia ya kunua wakina dada wanaouza miili ya maarufu kama dada poa ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali ya ngono.
Ushauri huo ulitolewa jana kwenye kikao cha baraza la madiwani la manispaa hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Mpanda kilichoongozwa na Meya wa Manispaa hiyo Willy Mbogo.
Awali katika kikao hicho Mwenyekiti wa kamati ya kudhibiti ukimwi Lucas Kanoni wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo alisema kuwa biashara ya akina dada ya kuuza miili yao imekuwa ni tishio kubwa hivi sasa katika Manispaa hiyo .
Alisema kuwa madada poa hao kwasasa wameanza kufanya biashara ya kuuza mili yao kwa kujishusha na kuanza kufanya ngono na wanafunzi wa shule hadi za msingi jambo ambalo ni hatari kwa watoto hao kutokana na kuwepo kwa magonjwa ya ngono kama ukimwi.
Kanoni alisema kuwa yapo maeneo mbalimbali katika Manispaa hiyo ambayo yamekuwa ni maarufu kwa biashara hiyo ambayo aliyataja kuwa ni mtaa wa Fisi ulioko katika Kata ya Majengo B ,M taa wa Simba ulioko Kata ya Majengo B, Kakese na Mwamkulu .
Naye diwani wa Kata ya Kashaulili John Matongo aliliambia baraza hilo la madiwani kuwa hivi sasa elimu ni muhimu ikatolewa kuanzia shule za msingi ili kuwaelimisha wanafunzi waweze kuacha kuwa wateja wao na pia kujikinga magonjwa ya ngono.
Alisema endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kutokana na kushamilikwa biashara hiyo upo uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa mitaa mingine ambayo haina sifa ya biashara hiyo ya dada poa kama ilivyo kwa mitaa ya simba na fisi .
Kwaupande wake meya wa Manispaa ya Mpanda Wily Mbogo alisema kuwa ni vema watoto waanze kufundishwa toka wakati wakiwa wadogo wakiwa mashuleni kutojihusisha na kufanya mambo ambayo hayalingani na umri wao kama vile kufanya ngono.
Alifafanua kuwa endapo kama hawatapewa elimu mapema ya kujiepusha na kufanya ngano wakiwa na umri mdogo upo uwezekano wa kupata maambukizi ya vvu.
Katika kikao hicho mkuu wa Wilaya ya Mpanda Lilian Matinga alisema kuwa kwa sasa Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa yenye maambukizo ya vvu kwa kiwango cha juu ya wastani wa Kitaifa .
Alisema maambukizi ya vvu kwa mkoa wa Katavi ni asilimia 5.9 wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 5.9 hivyo mkoa huo uko juu ya wastani wa maambukizi ya Kitaifa.
Aliongeza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu sasa wastani huo wa maambukizi umekuwa upo pale pale bila kushuka jambo ambalo ni hatari kwa wananchi endapo hawata badili tabia.
Ndiyo maana serikali imepanga kufanya utafiti kwenye mikoa mitano yenye maambukizi makubwa ya maambukizi ya vvu ambayo ni Songwe, Katavi Njombe ,Mbeya na Kigoma.
Mwisho