Na Israel Mwaisaka
Nkasi
MTOTO mwenye umri wa miaka minne amefariki dunia papo hapo baada ya basi lenye Namba za usajili T178 DHD lililokuwa likisafiri kutoka Kabwe wilayani Nkasi kuelekea mjini Sumbawanga mkoani Rukwa kuacha njia na kupindukaa huku abiria 25 wakijeruhi na tisa kati yao wakiwa ni majeruhi.
Akizungumzia tukio hilo afisa mtendaji wa kata ya Kabwe Jofrey Kuzumbi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea mei 5 majira ya saa 12 asubuhi katika eneo la Malimba katika kata hiyo ya Kabwe.
Alisema kuwa gari hilo lilikua limebeba abiria 43 na waliojeruhiwa ni 25 na kati yao tisa ni mahututi na wamekimbizwa katika hospitali teule ya wilaya Nkasi huku wengine wakipelekwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha waliyoyapata.
Alisema kuwa baada ya ajali hiyo kutokea mtoto wa kike aliyefahamika kwa jina la Beatrice Nyansio (4) alifariki papo hapo huku mzazi wake akipata majeraha.
Afisa mtendaji huyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi hilo na baada ya ajali hiyo dereva wa gari hilo aliyefahamika kwa jina moja tu la Moses alikimbia na mpaka sasa haijulikani alipo.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa George Kyando alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa bado uchunguzi wa ajali hiyo ikiwa ni pamoja na kuendelea kumsaka dereva wa gari hilo ambaye amekimbia ili aweze kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo mkabili.
mwisho
Wednesday, 6 June 2018
Kipindu pindu chaua 397
Na Gurian Adolf
Sumbawanga
HALI
ya ugonjwa wa kipindu pindu bado ni tete wilayani Sumbawanga mkoani
Rukwa ambapo idadi ya wagonjwa imeendelea kuongezeka ambapo hivi sasa
imefikia vifo 15 na wagonjwa 397 waliougua ugonjwa huo tangu ulipolipuka
tena Mei 6 mwaka huu.
Mganga
mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Fani Mussa akizungumza na mwandishi wa
habari hizi amesema kuwa ugonjwa huo bado haujaisha na watu wamekuwa
wakiendelea kuugua.
Alisema
kuwa mpaka kufikia jana jumla ya watu 397 wameugua kufa na wengine
kupona ambapo mpaka hivi sasa kuna wagonjwa saba ambao bado wapo wodini
wakitibiwa ugonjwa huo.
Mganga
mkuu huyo alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni wananchi kutofuata
kanuni bora za afya hasa kunywa maji yasiyosalama sambamba na
kutojisaidia kwenye vyoo.
Alisema
kuwa hivi sasa wakulima wanavuna mpunga na maji wanayotumia kwa kunywa
ni ya kwenye majaruba ambayo si salama kiafya kwakuwa hayajachemshwa na
baadhi yao wakijisaidia porini.
Dkt
Mussa alisema kuwa idara ya afya inajitahidi kutoa elimu lakini bado
wananchi hawafuati taratibu za kujikinga na ugonjwa huo licha ya kwamba
sheria kali pia zinatumika lakini bado ugonjwa huo unaendelea.
Alisema
katika kipindi cha November mwaka jana ugonjwa huo ulilipuka na
ulidhibitiwa ilipofika mwezi March mwaka huu lakini bila matarajio
ugonjwa huo ulilipuka tena mwezi mei mwaka huu na katika siku si nyingi
umeua watu 15 tofauti na mwaka jana ambapo watu 7 ndiyo waliopoteza
maisha.
Mwisho
Rukwa kujikita kwenye Alizeti
Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MKOA
wa Rukwa umejipanga kwaajili ya kuzalisha zao la alizeti ili
kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula unaotokea mara
kwa mara hapa nchini.
Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alisema hayo hivi karibuni wakati anazungumza na balozi
wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock ofisini kwake wakati akiwasilisha ombi la ushirikiano
baina ya mkoa wa Rukwa na nchi yake hali itakayo ongeza uzalishaji wa zao la alizeti mkoani humo na kupelekea
kuinua kipato cha wakazi wa mkoa wa huo.
alisema kuwa Kwa
mwaka 2016/2017 zililimwa hekta 47,862 za alizeti na kupatikana tani 53,470
ambayo ni chini ya kiwango kilichotakiwa kuzalishwa kutokana na tafiti
mbalimbali zilizofanywa kwa hekta 47,862 zikilimwa vizuri zinaweza
kupatikana tani 119,655 ambayo ni ongezeko la asilimia 55.
Wangabo
alisema kuwa nia ya kujikita katika kuzalisha alizeti kwa wingi ni
kuzalisha mafuta ya alizeti kwa wingi, kutengeneza ajira na
kuongeza viwanda ili kufikia nia ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi
wa viwanda.
Alisema kwa
mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Tanzania inatumia
Shilingi bilioni 189.6 kila mwaka kununua mafuta ya kula nje ya nchi
huku ikizalisha tani 91,000 ambayo ni sawa na asilimia 40 za mafuta hayo
tofauti na makadirio ya tani 200,000 hadi 300,000 ya uhitaji wa bidhaa
hiyo kwa mwaka kitu ambacho mkoa wa Rukwa umeiona fursa hiyo na hivyo umejipanga kujikita katika kilimo cha alizeti vizuri.
Mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alisema kuwa mkoa unatarajia kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la
Faida mali ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kukuza zao la alizeti
katika Mkoa wa Singida ili kuhamishia ujuzi huo katika Mkoa wa Rukwa.
Kwa upande wake balozi wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock alisema kuwa amefurahishwa sana na mikakati hiyo ya mkoa wa Rukwa kwa kuona umuhimu wa kutafuta zao mbadala la biashara katika Mkoa wa Rukwa ikiwa ni pamoja na kuinua kilimo cha mkoa na kuinua kipato cha wakulima wadogo na hatimae kuwatafutia namna ya kuongeza viwanda vidogo na kuongeza ajira.
Alisema
kuwa serikali ya nchi yake ipo tayari kutoa msaada wa hali na mali ili
mkoa huo uweze kufikia malengo hayo kitu cha muhimu ni kuendelea na
ushirikiano ili mikakati hiyo iweze kufanikiwa na kuleta tija kwa
wakulima pamoja na serikali kwa ujumla.
Mwisho
Saturday, 2 June 2018
Wanafunzi Nkasi sasa wapeana mimba
Na Gurian Adolf
Nkasi
IMEELEZWA vitendo vya kupeana mimba baina ya wanafunzi kwa
wanafunzi vimeshika kasi katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa hali inayochangia
kukwamisha jitihada za kukabiliana na mimba za utotoni wilayani humo.
Hayo yalielezwa jana na hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya
hiyo Ramadhan Rugemalila wakati akitoa mada katika mkutano wa siku moja wa
kupitia utekelezaji wa mpango kazi wa kuanzia mradi wa kuzuia mimba za utotoni
unaofadhiriwa na shirika la kimataifa la Plan International wa mwezi Januari hadi Juni na kuandaa mpango
kazi wa mwezi Julai hadi mwezi Desemba mwaka huu.
Alisema kuwa kutokana na elimu inayotolewa kwa wananchi
pamoja na adhabu kali za kisheria zinazotolewa hivi sasa vitendo vya watu
wazima kuwapa mimba watoto wa kike vimepungua badala yake vimeibuka vitendo vya
kupeana mimba wanafunzi kwa wananfunzi.
Rugemalila alisema kuwa hivi sasa mahakani zimejaa kesi za
mimba kwa wanafunzi ambazo idadi kubwa ni wanafunzi wamekuwa wakipeana mimba
hali ambayo inalazimu sasa mashirika ya kutoa elimu yaelekeze nguvu mashuleni
huenda mashirika yaliyopo yalijikita kutoa elimu kwa watu wazima na wakawasahau
wanafunzi.
Hakimu huyo mfawidhi alisema kuwa pia changamoto nyingine
iliyopo ni sheria inayotoa adhabu kwa mwanafunzi anayempa mwanafunzi wa kike
ujauzito kwani haitoi adhabu kali
isipokuwa inaelekeza kupelekwa katika magereza maalumu ya watoto ambako
anakwenda kuendelea na masomo hivyo kitendo hicho kinasababisha baadhi yao kuto
ogopa wakati mwanafunzi wa kike anapoteza fursa ya masomo.
Alisema kuwa pia ipo chanagamoto kwa baadhi ya kesi kukosa
ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani watuhumiwa ama baadhi ya mashahidi wakiwemo
waadhirika wa mimba za utotoni kutofika mahakamani hali inayosababisha baadhi
ya kesi kufutwa na watuhumiwa kuachiwa huru kitendo kinachosababisha wananchi
kuvitupia lawama vyombo vya sharia kuwa havitendi haki.
Kwaupande wake mratibu wa mradi wa kuzuia mimba za utotoni
wilayani Nkasi Frank Nestory alisema kuwa tangu mradi huo ulipoanza kutekeleza
wilayani humo kumekuwa na madiliko chanya kitendo kinachoonesha jamii hiyo
ilikosa elimu.
Alisema kuwa wapo baadhi ya wazazi walikuwa hawatambui kuwa
kumuozesha mtoto wake mdogo wa kike ni kosa kisheria kwani mlolo
huyo ni wakwake kwahiyo hakuna mtu anayeweza kumzuia kufanya hivyo mradi aamue
yeye mwenye mtoto.
Nestory alisema kuwa ni mtumaini yake mpaka mradi huo
utakapokuwa umefikia mwisho suala la mimba kwa watoto wilayani Nkasi litabaki
historia kutokana na elimu wanayoitoa sambamba na nmwitikio wa wananchi katika
kuunga mkono jitihada za kutokomeza ndoa za utotoni pamoja na mimba.
Mwisho
Subscribe to:
Posts (Atom)