Sunday, 17 December 2017

Siro awashukia wazazi

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MKUU wa jeshi la polisi nchini IGP Simon Siro amewatupia lawama baadhi ya wazazi nchini kuwa ndio chanzo cha watoto wao kupotea na kujiingiza katika makundi ya uhalifu kutokana na malezi mabovu ya kutowajali watoto hao. 

Aliyasema hayo juzi wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mkoani Rukwa waliotaka kujua sababu zilizopelekea idadi kubwa ya watoto wapatao1,300 kupotea katika eneo la Kibiti mkoani Pwani.

Alisema kuwa wapo baadhi ya wazazi ambao hawajali wala hawawajibiki ipasavyo katika malezi ya watoto wao hivyo kuwaacha bila kujua mienendo ya maisha yao ya kila siku,kitendo kinacho changia watoto kupotea. 

"utakuta mtoto anatoweka nyumbani na kwenda kusiko julikana ikiwemo kutafuta kazi za ndani ili ajipatie fedha na wazazi hawajali wanaona kawaida bila kujali kuwa ni mwanafunzi kitendo kinachochangia kuacha masomo,wakati alipaswa kuwepo shuleni ili ajitengenezee maisha yake ya  baadae"

Kamanda IGP Siro alisema watoto wanamahitaji yao ambayo wanapaswa kuyapata kutoka kwa wazazi pamoja na kusimamiwa, sasa wasipo patiwa ndiyo maana baadhi yao wanatoroka nyumbani na kwenda kusikojulikana wakiamini kuwa wanakwenda kujitafutia matokeo yake wanaacha shule na kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu ikiwemo ujambazi. 

Alitoa wito kwa wazazi wote nchini katika kuwajibika kwenye malezi ya watoto wao ikiwemo kupata elimu ambayo inatolewa bure na serikali ya awamu ya tano ili taifa lijekuwa na viongozi wazuri siku zijazo waliolelewa katika maadili bora.

Aidha kamanda IGP Siro alisema kuwa jitihada zinaendelea kufanyika na tayari baadhi ya watoto wamekwisha anza kupatikana lakini wazazi hawanabudi kutimiza wajibu wao wa malezi na kujali kuhusu watoto wao. 

Hata hivyo aliwaasa watendaji wa jeshi la polisi Kushirikiana vizuri na wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri kwa urahisi kwani dhamana waliyonayo ni kuwalinda raia na mali zao hivyo ni lazima wawahudumie vizuri raia wote ili wafurahie huduma za jeshi hilo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment