Thursday, 1 March 2018

Majambazi wateka mgodi waua,wapora dhahabu

Na Walter Mguluchuma
Katavi
WATU watatu  wanaosadikiwa  kuwa ni  majambazi walivamia machimbo ya   madini ya   dhahabu  ya Ifumile  Kijiji  cha  Isumamilomo  Tarafa ya  Nsimbo  Wilaya ya  Mpanda na kumuua mchimbaji   mmoja kwa  kumpiga   risasi tumboni  kwa  kutumia    bunduki ya   kivita  aina ya AK 47 nakisha  kujeruhi wengine watatu na kupora   dhahabu yenye uzito wa  zaidi  ya   Gramu 600,fedha  tasilimu shilingi milioni 1.5 na   mashine  mbili za kutafutia  dhahabu.
Kamanda  wa   Jeshi la  Polisi wa  Mkoa  wa  Katavi  Damas  Nyanda   aliwaambia  wandishi wa  habari  kuwa  tukio  hilo lilitokea  juzi  majira ya  saa 2 usiku  katika  machimbo.
 Alisema  siku  hiyo ya  tukio  majambazi hao  ambao  waliokuwa  watatu   walifika  katika  machimbo  ya  dhahabu ya  Ifumile yaliko  katika  Kijiji  cha  Isumamilomo  huku  wakiwa  wamejifunika  sura  zao  kininja na  kuwashambulia  kwa risasi wachimbaji na  wanunuzi wa  dhahabu  kwenye  machimbo  hayo .
Katika   shambulio  hilo   waliweza  kuwajeruhi wachimbaji wanne  katika   sehemu mbalimbali za mili yao   huku   baadhi ya  wachimbaji  waliokuwa  kwenye    eneo  hilo  waliweza  kusalimika  baada  ya kuwa  wamekimbilia  kwenye  vichaka.
  Kamanda  Nyanda  alimtaja aliyeuwa kwa  kupigwa  risasi  kuwa  ni Sita   Kalyalya (34Mkazi wa   Bariadi  Shiyanga   ambae  alipingwa  risasi ya  tumboni   na  mkononi  na aliyefariki dunia   muda  mfupi  baada ya  kufikishwa katika  Hospitali ya  Manispaa ya   Mpanda  wakati    akiwa   anapatiwa  matibabu.
Aliwataja pia waliojeruhiwa  kuwa ni   Joseph   Panya(34)  ambaye amejeruhiwa kwenye bega  la  kushoto  na  mguu wa kulia mwingine ni Mrisho   Rashid (21aliyejeruhiwa   mguuni  na     mkono  wake wa kulia  na Masunju  Mgulu  (28aliyejeruhiwa     mguu na  mkono wake  wa  kushoto .
Kamanda   Nyanda  alisema  majambazi hao watatu hao  baada ya  kuwajeruhi  wachimbaji hao  walipora  fedha   tasilimu   Tshs  1,500,000    Gramu  650 za  madini ya   dhahabu  na  mashine  mbili za  kutafutia  madini   na  kisha  kutokomea  kusiko julikana.
Mara  baada ya tukio  hilo  polisi  walifika  eneo  hilo  hata  hivyo  waliweza  kuokota   risas  24  na   maganda saba  ya  risasi zilizotumika   za   bunduki ya  kivita  aina ya AK  47 iliyotumika  kwenye  tukio  hilo.
  Alisema   Jeshi la  polisi  Mkoa  wa  Katavi  bado  linaendelea  kuwasaka    majambazi hao na alitoa  wito kwa  wananchi  kutoa  ushirikiano kwa  jeshi  hilo  kwa  kuwapatia  taarifa  zitakazowawezesha  kuwatia  nguvuni  watuhumiwa  watukio  hilo .
Kaimu   Mganga  Mkuu  wa  Hospitali ya  Manispaa ya  Mpanda  Dr  Jaffari Masanja  alisema  marehemu Kalyalya  alifariki muda  mfupi  baada  ya  kuwa   ametolewa kwenye chumba  cha upasuaji  ambako   alikuwa   akipatiwa  matibabu ya   kuunganishiwa  utumbo  wake  mkubwa   ambao  ulikuwa  umekatika  kutokana  na  kupigwa  risasi  tumboni .
 Alisema  majeruhi  Panya   na   Rashid wao   ambao  walikuwa  wamelazwa  katika  wodi  namba  moja wamepewa  rufaa na  wamesafirishwa  kwenda  katika  hospitali ya  Rufaa ya  Muhimbili  kwa  ajiri ya  matibabu  zaidi  baada  ya hali zao kuwa  mbaya  ambapo  majeruhi Masunju   Mgelu  yeye   amebaki  kwenye  hospitali  hiyo  huku  hali yake  ikiwa  inaendelea  vizuri.
Mwisho

No comments:

Post a Comment