Na Israel Mwaisaka
Nkasi
WAZIRI wa afya na ustawi Ummy Mwalimu amechukizwa na kitendo cha Hospitali teule ya wilaya mjini Namanyere NDDH kwa kushindwa kufuata kanuni za mkataba uliopo kati yao na serikali na kuitaka halmashauri ya wilaya Nkasi kupitia madiwani kuchukua hatua kama hari hiyo itaendelea.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa Rukwa iliyosomwa na mganga mkuu wa mkoa Rukwa Dkt,Boniface Kasululu ikulu ndogo wilayani Nkasi alisema kuwa amepata taarifa za kiutendaji zisizoridhisha katika hospitali hiyo teule na kuvunja mikataba waliyowekeana na serikali kitu ambacho ni kinyume chas sheria.
Alisema serikali inapeleka fedha nyingi katika hospitali hiyo sambamba na watumishi kadhaa wa serikali lakini taarifa alizonazo zimemvunja moyo na kuwapa jukumu madiwani kufuatilia ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua.
Waziri Ummy alifafanua kuwa kwa sasa mikataba yote ya namna hiyo itakuwa inafanywa na madiwani ili wawe na uwezo wa kuchukua hatua stahiki pale mambo yanapokwenda kinyume na mkataba waliowekeana.
Sambamba na hilo alizitaka halmashauri zote mkoani Rukwa kujenga hospitali zao za wilaya na kuwa mpango uliopo sasa ni halmashauri zote Nne zilizopo mkoani Rukwa kuhakikisha kuwa wanajenga hospitali za serikali za wilaya na kuwa hilo ndiyo litakuwa suluhisho la changamoto hizo wanazokumbana nazo kwenye ubia na hospitali za mashirika.
“serikali ni lazima iwe na hospitali zake na hizi za mashirika zitatumika pale itakapoonekana kuna uhitaji kulingana na eneo husika na idadi ya watu lakini sasa hospitali za serikali ni lazima ziwemo na hili ni lazima likamilike haraka sana’’ alisema Ummy
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa afya aliupongeza mkoa Rukwa kwa kufanikiwa kupunguza vifo vya kina Mama wajawazito kwa 95% na wajawazito wengi kuweza kujifungulia kwenye vituop vya kutolea huduma.
Alisema mpango wa serikali sasa ni kutaka kupunguza vifo vya kina mama wajawazito kwa asilimia kubwa na kuwa mkoa Rukwa umeonyesha njia ya kuweza kufanikiwa juu ya hilo na kuwa mkoa Rukwa una idadi ndogo ya watumishi wa afya lakini wamefanikiwa katika hilo na kuahidi kuwa katika ajira mpya watahakikisha wengi wa watumishi hao wanapelekwa mkoani Rukwa ili kuweza lkurahisha huduma hizo kwa Wananchi.
Alidai kuwa serikali kwa sasa imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana kwa urahisi zaidi na kwa kuliona hilo serikali imepanga kujenga vituo vya afya vitatu kwa kila wilaya na kwa Nchi nzima zitajengwa zahanati 500.
Na amedai kuwa kumetolewa muongozo sasa unaotaka zahanati ziongozwe na watu wenye elimu stahiki na kuacha kuwatumia Wahudumu wa afya na Wauguzi katika kuziongoza zahanati hapa nchini na kuwa hataki kuona tena jambo hilo likijirudia.
Waziri Ummy Mwalimu amemaliza ziara ya siku tatu mkoani Rukwa ambapo amekagua shughuli mbalimbali za afya katika mkoa Rukwa
Mwisho
No comments:
Post a Comment