Na Gurian Adolf
Kalambo
HALMASHAURI ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa imepiga maruku shughuli za uvuvi wa samaki pamoja na kuogelea katika ziwa Tanganyika mpaka hapo idara ya afya wilayani humo itakapo toa taarifa ya kumalizika kwa ugonjwa huo.
Uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwenye kijiji cha Samazi kilichopo mwambao wa ziwa hilo ambapo kijiji hicho kinakaliwa na wavuvi zaidi.
Akizungumzia marufuku hiyo Afisa uvuvu wa wilaya hiyo Wilbroad Kansapa alisema kuwa wavuvi ambao wamekuwa walifanya shughuli zake katika ziwa hilo wako hatarini kupata ugonjwa huo kutokana na kutochukua tahadhari ya kutosha kwani baadhi yao wamekuwa wakinywa na kuoga maji hayo kitendo ambacho ni hatari.
Alisema kuwa baadhi ya wavuvi na waogeleaji wanapokuwa wakifanya shughuli hizo katika ziwa hilo na kujikuta wakinywa maji kitendo ambacho ni hatari kwani hawawezi kujua kama Maji hayo yana vimelea vya ugonjwa huo.
Mpaka hivi sasa watu 18 wamekwisha ugua ugonjwa huo na ni mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Lina Protas(5) ndiyo aliyefariki dunia kwa ugonjwa huo na idara ya afya wilayani humo inafanya kila liwezekanalo katika kuhakikisha kuwa wanakabiriana na kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo katika halmashauri hiyo.
Afisa uvuvi huyo alisema kuwa wanajitahidi pia kudhibiti wavuvi kutoka katika nchi jirani ya Zambia hususani katika maeneo ya Mpulungu na Mbala ambao wanafika mpaka upande wa nchini Tanzania maeneo ambayo yana kipindu pindu kufanya shughuli za uvuvi ili kuzuia wasije pia wakapata ugonjwa huo na kuupeleka nchini mwao na hivyo kusababisha watu kuugua.
Kwa upande wake afisa uvuvi wa kata ya Samazi ambako mpaka hivi sasa ndio kuna ugonjwa huo Medadi Hosea alisema kuwa kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji vilivyopo katika kata hiyo wameweka sheria ndogo kuwa iwapo akikutwa mvuvi anavua samaki ama akiogelea ndani ya ziwa hilo atakamatwa na kulioishwa faini ya shilingi elfu 50,000.
Hata hivyo kuibuka kwa ugonjwa wa kipindu pindu katika kijiji hicho cha Samazi kumeonekana kumnyima raha mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelote Steven ambaye amaonekana kuwa karibu na wilaya hiyo zaidi kwa kufanya ziara na mikutano ya kutoa elimu katika kuhakikisha kuwa ugonjwa huo unadhibitiwa ili usienee katika sehemu nyingine huku akizingatia agizo la raisi John Magufuli kwa wakuu wa mikoa hapa nchini kuwa hataki kusikia kuwa wananchi wanapoteza maisha kwa ugonjwa huo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment