Sunday, 28 May 2017

Katavi washauriwa kusafiri kwa mabasi

Na Walter  Mguluchuma
Katavi

Wakazi Mkoani Katavi wametakiwa kuacha tabia ya kusafiri kwa kutumia maroli kwani kwa sasa Mkoa huo unayo mabasi ya kutosha yanayofanya safari zake kwenda katika Mikoa mingine ya hapa nchini.

Wito huo umetolewa na Afisa wa Mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini ( SUMATRA ) wa Mkoa wa Katavi Amani Mwakalebela wakati wa uzinduzi wa safari za mabasi ya Kampuni ya Adventure Connection yatakayo anza safari zake kutoka Mjini Mpanda Mkoani Katavi kwenda jijini Dar es salaam na uzinduzi huo ulifanyika katika stendi kuu ya mabasi yaendao Mikoani iliko katika Mtaa wa Mji Mwema mjini humo.

Alisema kutokana na kuboreshwa kwa barabara za Mkoa huo kumesababisha wenye mabasi wahamasike na kupeleka mabasi yao mkoani humo, hivyo ni vema wakazi wa Mkoa huo wakasafiri kwa mabasi badala ya kusafiri kwa maroli.

Mwakalebela aliwataka abiria waache tabia ya kuwashangilia madreva wanao endasha mabasi kwa kwendo kasi kwani kufanya hivyo wanahatarisha usalama wao na Mali zao.

Awali kabla ya uzinduzi huo wa safari za mabasi ya kampuni ya Adventure wajumbe wa kamati ya usalama barabarani walitoa elimu kwa madreva pamoja na abiria.

Naye Mwenyekiti wa usalama barabarani wa Mkoa wa Katavi Nassor Arfi aliwasisitiza wamiliki wa mabasi kutoza nauli zile ambazo zimepangwa na SUMATRA.

Aliipongeza kampuni hiyo kwa kuzindua safari zake za kutoka Mpanda kuelekea jijini Dares salaam kwani itakuwa ni mkombozi kwa wasafiri ambao walikuwa wakitumia siku mbili hadi tatu kuweza kufika Dares Salaam lakini sasa watakuwa wanatumia siku moja tu.

Meneja wa Kampuni ya Adventure Nassor Ally alisema kuwa kampuni hiyo imejipinga na itaendelea kuboresha huduma kwa ajiri ya wateja wake kila wakati.

Alisema watakuwa wakifanya safari hizo mara tatu kwa wiki na mabasi yao yatakuwa yakipita katika Mikoa ya Tabora , Singida, Dodoma, Morogoro hadi Dares Salaam.

Mwisho

No comments:

Post a Comment