Waziri Mkuu wa serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa, Abdullah al-Thani, ameponea chupuchupu kuuawa baada ya msafara wake kushambuliwa kwa risasi katika mji wa Tobrouk, mashariki mwa nchi.
Waziri Mkuu huyo alikuwa kitoka bungeni alikokuwa akijibu maswali ya wabunge wakati genge la watu wenye silaha lilipoufuata msafara wake na kuanza kuumiminia risasi. Habari zinasema kiongozi huyo amenusurika lakini mlinzi wake mmoja amejeruhiwa vibaya. Baraza la mawaziri la serikali ya al-Thani limelaani shambulizi hilo na kusema watekelezaji wa jinai hiyo huenda walilipwa na serikali bandia iliyoko Tripoli ili kumuua Waziri Mkuu al-Thani.
Hii si mara ya kwanza kwa wanamgambo wenye silaha kuwahangaisha
viongozi wa Libya. Mwaka 2013, Waziri Mkuu wa wakati huo, Ali Zeidan,
alitekwa nyara na watu wenye silaha na kisha kumuachilia huru baadaye.
Libya inakabiliwa na mkwamo wa kisiasa kwani nchi hiyo ya kaskazini mwa
Afrika ina serikali mbili na mabunge mawili ambayo yanayopigania uongozi
na satua katika nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment